Pages

Pages - Menu

Tuesday, 11 August 2015

UPAKO NA NGUVU ZA DAUDI KUMUUWA SIMBA


***SIRI YA NGUVU ZA DAUDI***



Daudi alikuwa mdogo kati ya wana nane, wa mwisho, mdogo, aliyechukuliwa kama hana umuhimu, aliyekuwa akifanya kazi isiyo na umuhimu, kazi isiyoheshimika, kazi isiyopendwa na kaka zake wote; kazi ya kuchunga kondoo.

Hapa somo ni kuwa, Mungu huwa haangalii sana kitu tunachofanya kama jinsi tunavyokifanya hicho kitu. Sisi wote tuna kitu cha kuchunga, na kila mmoja ana wajibu kwa kitu fulani.

Mungu anatutazama: jinsi unavyotunza nyumba au chumba chako, jinsi unavyofanya kazi au biashara zako, jinsi unavyowatreat rafiki zako, ndugu zako na wazazi wako, jinsi unavyoenenda ukiwa mbali na familia yako au mbali na wazazi wako . Je unadanganya? Je unawaambia watu ukweli au unawaambia kile wanachotaka kusikia ili wakuruhusu kufanya kile unachotaka kufanya? Je ni mangapi unayoyasema unamaanisha?

Wakati wa kuinuliwa kwa Daudi, walijua mahali hasa alipokuwepo na nini alikuwa anafanya kwa uaminifu, uhakika na kwa kujituma.

Angalia jinsi mtazamo wa Mungu ulivyotofauti na mtazamo wa mwanadamu; mtu aliyechukuliwa kuwa hana umuhimu sasa ni muhimu miongoni mwao. (1 Samweli 16:7)

Hawakumfikiria, hawakuwa na wazo juu ya Daudi, lakini sasa wakasimama juu wakisubiri kuja kwake. “Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja” (1 Samweli 16:11)

Kumbuka; mtu nainua na kukuza vipaji, uwezo na kadhalika, lakini Mungu anainua na kukuza utu wa mtu. Ninasoma mara nyingi ‘post’ na ‘status’ za rafiki zangu kuwa wameketishwa na wakuu.....Mithali 18:16 imeandikwa “ Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu.”

Leo naomba niwaambie kuwa; zawadi yako inaweza kukuleta mbele ya watu wakuu, lakini ni utu ambao utakuwezesha wewe kuendelea kukaa au kuketi huko. MUNGU ANAANGALIA UTU... Zawadi ya Yusufu ilimleta mbele ya Farao, lakini ni utu wake uliomfanya kuwa Waziri Mkuu wa Misri.

Mungu akamwambia Samweli; nimejipatia mfalme katika wana wa Yese (1 Samweli 16:1)
Kwa mwanadamu kumpata mtu huja baada ya kumtazama, kumwangalia, kumwona, kumkagua, kumchunguza, kumpeleleza, kumfikiria, kupendezwa naye na kuamua. Tena wengi tunapomtazama mtu tunaangalia na sura. Lakini MUNGU HAANGALII SURA WALA UMBILE...MUNGU HUTAZAMA MOYO... Katika 1 Samweli 16:7 tunasoma “Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa.”

Kimsingi hapa Mungu anasema; “Nimekuwa nikiwaangalia wana Yese, na nimekuwa nikiwachunguza na kujifunza jinsi wanavyofikiri na jinsi wanavyoenenda, na jinsi walivyo wakati hakuna mtu anayewatazama, na nimemchagua mmoja wao kuniwakilisha mimi.”

Ubora sio tukio la mara moja. Je tunapomwona Daudi akimuua Goriati tunafikiri kwamba hapo ndipo alipokuwa bora? Kuwa bora sio kufanya jambo kubwa vizuri; kuwa bora ni kufanya kila kitu kidogo vizuri.

Ubora wa kweli hauonekani katika mambo makubwa tunayoyafanya, bali katika mambo madogo madogo tunayoyafanya vizuri.

Watu bora hufanya kwa mfululizo kile kitu ambacho wengine hufanya mara mojamoja tu.

Taji haimfanyi mtu kuwa mfalme, bali hubainisha tu ufalme wa mtu.

“Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye (1 Samweli 16:12) na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile.” (1 Samweli 16:13)

Sasa tunaona SIRI YA NGUVU ZA DAUDI

Kwanza; Alikuwa na Utu
Utu ni kile tunachojisemea kutuhusu sisi wenyewe, na kile tunachoruhusu wengine kukiona juu yetu, Utu ni vile tulivyo wakati hakuna mtu anatuangalia.

Pili; Alikuwa na Upako wa Roho Mtakatifu.
Mungu anatafuta Madaudi na Majoshua awape upako kwa Roho wake Mtakatifu
Je, utakuwa mmoja wao? Daudi alikuwa mdogo wa nane, Alikuwa namba 8 ambayo kwa mwendelezo ni namba ya mwanzo mpya. Mungu anataka kufanya jambo jipya...

Tatu; Daudi Aliheshimu Ahadi.
Katika 1 Samweli 17:26 tunasoma “Je Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai? Halafu mbele pale mstari wa 37 “Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu.

Alikuwa ni huyuhuyu David mdogo, mchunga kondoo, mapakwa mafuta wa Roho Mtakatifu aliyewaua simba na dubu, ambaye alikuwa mbeba silaha wa Sauli, ambaye alipiga kwa ustadi kinubi na alimfukuza roho mchafu mbali na Sauli, ambaye alisimama peke yake dhidi ya Mfilisti bingwa akamwua kwa kombeo na jiwe, na kukata kichwa chake kwa upanga wake mwenyewe, na kulitoa taifa kutoka mikononi mwa adui.

Lakini Daudi alishakufa na kwenda, kilichobaki ni rekodi za maisha yake na katika rekodi za maisha yake tunaona SIRI YA NGUVU ZAKE.

Utu huanza na uamuzi wa kufanya maamuzi yanayompa utukufu Mungu katika maisha.

Je, mtazamo wako unampa Mungu utukufu? Je, mawazo yako yanampa Mungu utukufu? Je, mambo unayo yasikiliza na kuyaangalia yanampa Mungu utukufu? Je, uhusiano wako na mke, mpenzi au mchumba wako unampa Mungu utukufu?

Utu ni sehemu yetu, upako ni kazi ya Mungu.
Hebu kuwa kama Daudi na kumpa Mungu kitu cha kutia upako.

Kuna Goriati na baadhi ya simba na dubu ambao wanatakiwa kuuwawa leo, na Wewe ni chaguo la Mungu kwa ajili ya kazi hiyo na kwa upako wa Mungu juu ya maisha yako unaweza kumwangusha chini.

Jifunze kwa Daudi leo na Mungu atakuwa nawe siku zote!

No comments:

Post a Comment