Unyakuo Wa Kanisa Na Nyakati Za Mwisho
Yesu alipotembea hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, aliwaambia wanafunzi Wake waziwzi kabisa kwamba angeondoka kisha angerudi kuwachukua sikumoja. Wakati wa kurudi, angekwenda nao mbinguni. Kitu hiki siku hizi kinatiwa “Unyakuo.” Kwa mfano: Usiku ule kabla hajasulubiwa, Yesu aliwaambia hivi mitume Wake waaminifu kumi na moja:Msifadhaike mioyoni mwenu. Mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi. Kama sivyo, ningaliwaambia, maana naenda kuwaandalia mahali. Basi, mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. (Yohana 14:1-3. Maneno mepesi kukazia).Kilicho wazi katika maneno ya Yesu ni uwezekano wa kurudi Kwake wakati wale mitume wakiwa bado hai. Ukweli ni kwamba, baada ya kusikia maneno ya Yesu, wangeweza kudhani tu kwamba atarudi kuwachukua wakiwa bado hai.
Tena, Yesu aliwaonya wanafunzi Wake mara nyingi sana kwamba wawe tayari kwa ajili ya kurudi Kwake. Hapo tena, uwezekano wa Yeye kurudi wakiwa hai ulikuwepo (ona mfano katika Mathayo 24:42-44).
Kurudi Kwa Yesu Upesi Katika Nyaraka
Mitume walioandika zile barua za Agano Jipya walithibitisha imani yao kwamba Yesu angeweza kurudi wakati wa maisha ya wasomaji wa barua zao. Kwa mfano: Yakobo aliandika hivi:Kwa hiyo ndugu, vumilieni hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani. Huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia (Yakobo 5:7, 8. Maneno mepesi kukazia).Yakobo asingekuwa na haja ya kuwashauri wasomaji wake kuvumilia kuhusu kitu ambacho kisingetokea maishani mwao. Yeye aliamini kwamba kuja kwa Bwana “kunakaribia.” Kimantiki, Yakobo aliandika barua yake wakati kanisa lilipokuwa linapitia mateso makali (ona Yakobo 1:2-4), wakati ambapo waamini wangetamani sana kurudi kwa Bwana wao.
Paulo vile vile aliamini kwamba Yesu angeweza kurudi wakati wa maisha ya wenzake. Anaandika hivi:
Lakini ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi farijianeni kwa maneno hayo (1Wathes. 4:13-18. Maneno mepesi kukazia).[1]Kutokana na hayo tunajifunza pia kwamba wakati Yesu atakaporudi kutoka mbinguni, miili ya waamini waliokufa itafufuliwa, kisha, pamoja na waamini walio hai wakati wa kuja Kwake, “kunyakuliwa ili kumlaki Bwana hewani” (Unyakuo). Kwa kuwa Paulo naye alitaja kwamba Yesu angewaleta wale waliokufa “ndani Yake” kutoka mbinguni, tunachoweza kusema ni kwamba wakati wa Unyakuo, roho za waamini walioko mbinguni zitaunganishwa na miili yao iliyofufuliwa punde tu.
Petro naye aliamini kwamba kuja kwa Kristo kulikuwa karibu sana, alipoandika barua yake ya kwanza kabisa.
Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. …Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia,basi iweni na akili, mkeshe katika sala. … Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe (1Petro 1:13; 4:7, 13. Maneno mepesi kukazia).[2]Na Yohana naye, alipoandika barua zake kwa makanisa, aliamini kwamba mwisho ulikuwa karibu, na kwamba wasomaji wa siku zake wangeona kurudi kwa Yesu.
Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. … Na sasa watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake. … Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu (1Yohana 2:18, 28; 3:2, 3. Maneno mepesi kukazia).
Kukawia Kwake
Tukitazama nyuma miaka elfu mbili, tunatambua kwamba Yesu hakurudi mapema kama mitume Wake walivyotazamia. Hata katika siku zao, kuna waliokuwa wameanza kuwa na mashaka kama Yesu angerudi, kutokana na muda ulivyokuwa umepita tangu aondoke. Kwa mfano: Maisha ya Petro hapa duniani yalipokaribia kumalizika (ona 2Petro 1:13, 14), Yesu alikuwa hajarudi bado. Basi, Petro aliwaandikia waliokuwa na mawazo ya mashaka hivi, katika barua yake ya mwisho:Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika sikuza mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, na kusema, ‘Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.’ Maana hufumba macho yao wasione neno hili yakuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji kwa neno la Mungu. Kwa hayo dunia ile ya wakati ule ioligharikishwa na maji, ikaangamia. Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. Lakini wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea” (2Petro 3:3-10).Petro anathibitisha kwamba kukawia kurudi kwa Yesu ni kwa sababu ya upendo na rehema na huruma Zake – anataka kutoa nafasi zaidi watu watubu. Lakini anasema pia kwamba hakuna mashaka yoyote – Yesu atarudi. Na atakaporudi, atakuja akiwa na ghadhabu kubwa.
Vile vile Maandiko yako wazi kabisa – kama tutakavyo-ona – kwamba kurudi kwa Kristo kwa ghadhabu kutatanguliwa na miaka ya dhiki isiyo na kifani ya dunia nzima, na kumwagwa kwa hasira ya Mungu juu ya waovu. Sehemu kubwa ya Kitabu cha Ufunuo inasema kuhusu kipindi hicho kinachokuja. Kama tutakavyoona baadaye katika mafunzo yetu, Maandiko yanaonyesha kwamba itakuwepo miaka saba ya dhiki, hapo baadaye. Hakuna shaka yoyote kwamba Unyakuo wa kanisa utafanyika wakati fulani katika hiyo miaka saba, au karibu na hiyo miaka saba.
Je, Unyakuo Ni Lini Hasa?
Swali ambalo mara nyingi linawagawa Wakristo ni wakati hasa wa Unyakuo. Kuna wanaosema kwamba Unyakuo utatokea kabla ya ile miaka saba ya dhiki. Kwa maana hiyo, unaweza kutokea wakati wowote. Wengine wanasema utatokea katikati ya ile miaka saba ya dhiki. Na wengine tena wanasema utatokea punde tu baada ya dhiki ya miaka saba kufika katikati. Na kuna wengine nao wanaosema kwamba Unyakuo utatokea wakati wa Yesu kurudi na ghadhabu nyingi, mwishoni mwa kipindi cha Dhiki.Hilo si swala la kugawanyikia, na makundi yote manne yanapaswa kukumbuka kwamba yote yanakubali kwamba Unyakuo utatokea wakati fulani katika kipindi hicho cha baadaye cha dhiki ya miaka saba, au karibu nacho. Hilo ni dirisha dogo sana katika upana wa miaka maelfu ya historia. Hivyo, badala ya kugawanyika kutokana na kutokubaliana kwetu, ni afadhali tufurahie makubaliano yetu! Tena, si kitu tunaamini nini maana haitabadilisha kitakachotokea.
Baada ya kusema hayo, sina budi kusema kwamba, kwa miaka ishirini na mitano ya kwanza katika maisha yangu ya Kikristo, niliamini kwamba Unyakuo utatokea kabla ya Dhiki ile ya miaka saba. Niliamini hivyo kwa sababu ndivyo nilivyofundishwa, na pia kwa sababu sikutaka kupitia mambo ninayosoma habari zake katika Kitabu cha Ufunuo! Ila, nilipoendelea kujifunza Maandiko, nilianza kupata mtazamo tofauti. Hebu kwa pamoja tutazame Biblia inavyosema, na tuone tutafikia maamuzi gani. Hata kama sitafanikiwa kukushawishi ujiunge na upande wangu, hebu tuendelee kupendana!
Mafundisho Pale Mlima Wa Mizeituni
Hebu tuanze kwa kutazama sura ya 24 ya Injili ya Mathayo, sehemu ya Maandiko ambayo ni ya msingi sana kwa habari ya matukio ya nyakati za mwisho na kurudi kwa Yesu. Pamoja na sura ya 25, sehemu hiyo huitwa Mafundisho Pale Mlima Wa Mizeituni, kwa sababu sura hizo mbili ni taarifa ya mahubiri ambayo Yesu alitoa kwa baadhi ya wanafunzi Wake wa karibu sana[3] hapo mlimani. Tunaposoma mafundisho hayo, tutajifunza kuhusu matukio mengi ya nyakati za mwisho, nasi tutaona uwezekano wa wanafunzi wa Yesu kufikiri muda wa Unyakuo ni upi, waliposikia mafundisho yenyewe.Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni. Wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. Naye akajibu akawaambia, ‘Hamyaoni haya yote? Amin nawaambieni, halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.’Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha wakisema, ‘Tuambie! Mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?’ (Mathayo 24:1-3).Wanafunzi wa Yesu walitaka kujua habari za wakati ujao. Sana sana walitaka kujua majengo ya hekalu yangebomolewa lini (kama Yesu alivyokuwa ametabiri) na ishara gani ingeonyesha wakati wa kurudi Kwake na mwisho wa wakati.
Ukilitazama hivyo, tunajua kwamba majengo ya hekalu yalibomolewa kabisa mwaka wa 70 B.K. na jemadari Tito, akiongoza majeshi ya Kirumi. Pia tunajua kwamba Yesu bado hajarudi kujichukulia kanisa Lake, kwa hiyo, hayo matukio mawili hayafuatani, wala hayatokei wakati mmoja.
Yesu Ajibu Maswali Yao
Inaonekana kwamba Mathayo hakuandika jibu la Yesu ka swali la kwanza, kuhusu kuharibiwa kwa majengo ya hekalu baadaye. Ila, Luka alifanya hivyo katika Injili yake (ona Luka 21:12-24). Katika Injili ya Mathayo, Yesu alianza moja kwa moja kuzungumza kuhusu ishara ambazo zingetangulia kurudi Kwake mwisho wa wakati.Yesu akajibu akawaambia, ‘Angalieni mtu asiwadanganye [ninyi]. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni [ninyi] msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifal na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu.’ (Mathayo 24:4-8. Maneno mepesi kukazia).Kutokana na jinsi mahubiri hayo yalivyoanza, ni dhahiri kwamba Yesu aliamini kwamba hao wanafunzi Wake wa karne ya kwanza wangekuwa hai wakati ishara hizo zinazotangulia kurudi Kwake zinapotendeka. Ona anasema nao moja kwa moja, kibinafsi. Katika sura hii ya 24, Yesu anasema na wanafunzi Wkae moja kw amoja zaidi ya mara ishirini. Basi, wasikilizaji Wake wote wangeamini kwamba wataishi na kuona hayo yote ambayo Yesu ametabiri.
Lakini ni kweli kwamba wanafunzi wote waliomsikiliza Yesu siku hiyo wamekufa siku nyingi sana. Ila, tusidhani kwamba Yesu alikuwa anawadanganya. Yeye Mwenyewe hakujua wakati atakaporudi (ona Mathayo 24:36). Kweli ilikuwa inawezekana kwa wale waliosikiliza mafundisho Yake pale Mlima wa Mizeituni kuwa hai wakati wa kurudi Kwake.
Kilichokuwa cha msingi kabisa kwa Yesu ni kwamba wanafunzi Wake wasidanganywe na makristo wa uongo, kama itakavyokuwa katika siku za mwisho. Tunajua kwamba Mpinga Kristo mwenyewe atakuwa kristo wa uongo, na atadanganya dunia kwa sehemu kubwa. Watuw atamhesabu kuwa mwokozi mzuri sana.
Yesu alisema zitakuwepo vita, njaa na matetemeko, lakini pia alionyesha kwamba hayo matukio si ishara za kurudi Kwake bali ni “mwanzo wa utungu” tu. Ni salama kusema kwamba matukio hayo yamekuwepo kwa miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita. Ila, anachosema Yesu baada ya hapo ni kitu ambacho hakijatokea.
Dhiki Inaaza Katika Dunia Nzima
Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukuwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja (Mathayo 24:9-14. Maneno mepesikukazia).Hapa tena – kama ungewauliza wale waliomsikiliza Yesu siku hiyo swali hili: “Je, mnatazamia kuwa hai ili kuona kutimia kwa mambo hayo?” bila shaka wangejibu ndiyo kwa uhakika sana, maana Yesu alisema nao moja kwa moja.
Kama tulivyosoma – mara tu baada ya “utungu” kuna tukio ambalo kweli halijatokea, la wakati wa Wakristo duniani kote kuteswa. Tutachukiwa na “mataifa yote”. Yesu alikuwa anazungumza juu ya wakati fulani ambapo hayo yangetokea – si kipindi cha jumla cha miaka mia nyingi, maana alisema hivi baada ya hayo, “Ndipo wengi watakapojikwaa,nao watasalitiana na kuchukiana.”
Bila shaka anachosema hapo kinahusu kurudi nyuma kwa waamini Wakristo ambao baada ya hapo watawachukia waamini wengine, maana wasioamini hawawezi “kuanguka,” tena, wanachukiana tayari. Basi, mateso ya dunia nzima yatakapoanza, kutakuwa na kurudi nyuma kwa watu wengi wanaodai kwamba ni wafuasi wa Kristo. Kama ni wakweli au ni waamini bandia – yaani kondoo au mbuzi – wengi sanawataanguka, nao watafichua majina ya waamini wengine kwa watesaji, wakiwachukia wale waliodai kuwapenda. Matokeo ni kwamba kanisa duniani kote litasafishwa.
Halafu tena kutakuwa na ongezeko la manabii wa uongo, na mmoja anatajwa sana katika kitabu cha Ufunuo kuwa mwenzake mpinga Kristo (ona Ufunuo 13:11-18; 19:20; 20:10). Maasi yataongezeka na kufikia mahali pa kumaliza kabisa upendo kidogo utakaokuwa umesalia mioyoni mwa watu, na wenye dhambi watakuwa wabaya kukithiri.
Wafia Dini Na Watakaosalia
Ingawa Yesu alitabiri kwamba waamini watapoteza maisha yao (ktk 24:9), si wote, maana aliahidi kwamba wale watakaovumilia mpaka mwisho wataokolewa (ona 24:13). Yaani, kama hawataruhusu wadanganywe na wale makristo wa uongo au manabii wa uongo, na kama watashinda jaribu la kuacha imani yao na kuanguka, wao wataokolewa na Kristo wakati anaporudi ili kuwakusanya mawinguni. Huu wakati wa dhiki baadaye pamoja na ukombozi wake ulifunuliwa kidogo kwa nabii Danieli pia. Yeye aliambiwa hiviNa kutakuwa wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile. Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele (Danieli 12:1, 2).Wokovu bado utatolewa kwa neema hata katika siku hizo, maana Yesu aliahidi kwamba Injili itahubiriwa kwa mataifa yote, kutoa nafasi moja ya mwisho ya kutubu, ndipo mwisho utakapokuja.[4] Tunasoma kitu katika Kitabu cha Ufunuo ambacho kinaweza kuwa kutimizwa kwa ahadi ya Yesu.
Kisha nikaona malaika mwingine akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injli ya milele, awahubirihao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa. Akasema kwa sauti kuu, ‘Mcheni Mungu na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji’. (Ufunuo 14:6, 7. Maneno mepesikukazia).Kuna wanaodhani kwamba sababu ya malaika kuhubiri Injili wakati huo ni kwamba, kufikia hapo katika kipindi cha dhiki ya miaka saba, Unyakuo utakuwa umetokea na waamini wote watakuwa wameondoka. Lakini, hayo ni mawazo tu.
Mpinga Kristo
Nabii Danieli alifunua kwamba mpingakristo atakuwa na nafasi katika hekalu la Yerusalemu litakalojengwa upya, katikati ya ile miaka saba ya dhiki, na kujitangaza kwamba ni Mungu (ona Danieli 9:27 – tutajifunza baadaye). Tukio hili ndilo Yesu anazungumzia alipoendelea kufundisha pale Mlima wa Mizeituni, kama ifuatavyo:Basi, hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi nyuma kuchukua nguo yake. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.[5] Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo (Mathayo 24:15-22).Hayo ni maelezo yaliyo dhahiri zaidi kuhusu dhiki ambayo Yesu alizungumzia mapema (ktk 24:9). Wakati mpingakristo atakapotangaza kwamba yeye ni Mungu kutoka hekalu la Yerusalemu, mateso yasiyofikirika yatatokea dhidi ya wanaomwamini Yesu. Kwa kujitangaza kwamba yeye ni Mungu, mpingakristo atatazamia kilamtu kutambua uungu wake. Basi, wafuasi wote wa kweli wa Kristo watakuwa maadui wa taifa, watu wa kusakwa na kuuawa. Ndiyo sababu Yesu aliwaambia waamini wa Uyahudi wakimbilie milimani bila kukawia, wakiomba kwamba kutoroka kwao kusizuiwe na sababu yoyote ile.
Wazo langu ni kwamba ingekuwa vizuri kwa waamini wote duniani kukimbilia maeneo yaliyofichika wakati huo, maana tukio hilo litatangazwa duniani kote kwa njia ya televisheni. Maandiko yanatuambia kwamba dunia nzima itadanganywa na mpingakristo na kudhani yeye ndiye Kristo wao, nao watampa mamlaka na heshima zote. Atakapojitangaza kwamba ni Mungu, watamwamini na kumwabudu. Atakaponena makufuru dhidi ya Mungu wa kweli – Mungu wa Wakristo – atashawishi dunia yote iliyodanganyika ili kuwachukia wale wanaokataa kumwabudu (ona Ufunuo 13:1-8).
Yesu aliahidi ukombozi kwa ajili ya watu Wake mwenyewe kwa “kukatisha” hizo siku za dhiki, vinginevyo, “asingeokoka mtu yeyote” (24:22). Huko “kukatizwa” siku hizo Naye “kwa ajili ya wateule” bila shaka ni kitu kinachohusu Yeye kuwakomboa wakati atakapoonekana na kuwakusanya mawinguni. Yesu hata hivyo hatuambii hapa kwamba ukombozi huo utatokea muda gani baada ya mpingakristo kujitangazia uungu.
Vyovyote vile – tunarudia kusema hapa tena kwamba Yesu aliwaacha wasikilizaji Wake siku hiyo wakiwa wanajua kwamba wangeishi na kumwona mpingakristo akitangaza uungu wake, na kupigana vita na Wakristo. Hili linapingana kabisa na wazo la wale wanaosemakwamba waamini watanyakuliwa kabla ya tukio hilo. Kama ungemwuliza Petro, Yakobo au hata Yohana kwamba Yesu angerudi kuwaokoa kabla ya tamko la mpingakristo kwamba ni Mungu, wangekujibu, “Si hivyo”.
Vita Dhidi Ya Watakatifu
Katika sehemu zingine, Maandiko yanatabiri juu ya mateso ya mpingakristo kwa waamini. Kwa mfano: Yohana alifunuliwa, naye akaandika hivi katika kitabu cha Ufunuo:Naye [mpingakristo] akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa (Ufunuo 13:5-7. Maneno mepesi kukazia).Ona hapo kwamba mpingakristo atapewa “uwezo wa kufanya kazi yake” kwa miezi arobaini na mbili, au, miaka mitatu na nusu kamili. Huu ndiyo wakati unaoitwa nusu ya wakati wa kipindi cha Dhiki ya miaka saba. Ni sawa kabisa kufikiri kwamba ni ile miezi arobaini na mbili ya mwisho ya Dhiki, ndipo mpingakristo atakapopewa “uwezo wa kufanya kazi yake,” kwa sababu mamlaka yake yataondolewa kabisa wakati Kristo atakaporudi kufanya vita naye na majeshi yake wakati wa kumalizika kwa Dhiki.
Ni dhahiri kwamba “uwezo wak ufanya kzi yake” kwa miezi arobaini na mbili maan ayake ni mamlakamaalum, maana mpingakristo atapewa mamlaka kiasi fulani na Mungu katika wakati wake wa kumiliki. Haya “mamlaka maalum ya kufanya kazi” yanaweza kuwa ni muda atakaopewa wa kuwashinda watakatifu, maana, tunasoma hivi katika kitabu cha Danieli:
Nikatazama, na pembe iyo hiyo [mpingakristo] ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; hata akaja huyo mzee wa siku [Mungu], nao watakatifu wake Aliye Juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme. … Naye [mpingakristo] atanena maneno kinyume chake Aliye Juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye Juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati (Danieli 7:21, 22; 25. Maneno mepesi kukazia).Danieli alitabiri kwamba watakatifu wangetiwa mikononi mwa mpingakristo kwa “wakati, nyakati, na nusu wakati.” Maneno hayo yaeleweke kwamba ni miaka mitatu na nusu, kama utafananisha na Ufunuo 12:6 na 14. Tunaambiwa katika Ufunuo 12:6 kwamba mwanamke fulani ambaye ni mfano, atapewa mahali pa kujificha nyikani ili “atunzwe na kulishwa” huko kwa muda wa siku 1,260, ambazo ni sawa na miaka mitatu na nusu kwa mwaka wenye siku 360. Kisha, mistari nane baadaye, anatajwa tena, na wakati huo inasemekana atapewa mahali nyikani ili “atunzwe na kulishwa” kwa “wakati, nyakati, na nusu ya wakati.” Basi, “wakati, nyakati, na nusu ya wakati” ni sawa na zile siku 1,260, au miaka mitatu na nusu.
Kumbe katika mantiki hii, neno “wakati” maana yake mwaka, na “nyakati” maana yake miaka miwili, na “nusu ya wakati” maana yake nusu mwaka. Lugha hii ya ajabu inayopatikana katika Ufunuo 12:14 bila shaka ina maana kama katika Danieli 7:21. Basi, sasa tunajua kamba watakatifu watatiwa mikononi mwa mpingakristo kwa miaka mitatu na nusu, ambao ndiyo muwa ule ule tunaoambiwa katika Ufunuo 13:5 kwamba mpingakristo atapewa “uwezo wa kufanya kazi yake.”
Mimi nadhani vipindi hivyo viwili vya miezi arobaini na mbili vinafanana. Kama vitaanza wakati wa mpingakristo kujitangaza kwamba ni Mungu katikati ya ile Dhiki ya miaka saba, basi ni kwamba watakatifu watatiwa mikononi mwake kwa miaka mitatu na nusu inayofuata, na Yesu atawakomboa atakapotokea mawinguni na kuwakusanya waende Naye wakati huo, au karibu na mwisho wa hiyo Dhiki. Lakini, kama hiyo miezi arobaini na mbili inaanza wakati mwingine katika kipindi cha Dhiki ya miaka saba, basi inatubidi tukubali kwamba Unyakuo utatokea wakati fulani kabla ya mwisho wa Dhiki ya miaka saba.
Tatizo la hoja hiyo ya mwisho ni kwamba inabidi watakatifu watiwe mikononi mwa mpingakristo kabla ya kuingia hatarini na kuhitaji kukimbilia milimani wakati anapojitangaza kuwa Mungu. Hilo ni gumu.
Tatizo la hoja ile ya kwanza ni kwamba watakatifu watakuwepo duniani bado wakati Mungu atakapokuwa anamimina hukumu duniani, tunazosoma katika kitabu cha Ufunuo. Tutatazama ugumu huo baadaye. Tuendelee na Mafundisho ya Mlima wa Mizeituni.
Masiya Wa Uongo
Ndipo Yesu akafafanua zaidi kwa wanafunzi Wake umuhimu wa kutodanganywa na habari kuhusu maKristo wa uongo.Wakati huo mtu akiwaambia, ‘Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu, wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai (Mathayo 24:23-28).Ona tena hapa jinsi Yesu anavyosema na wanafunzi moja kwa moja. Wasikilizaji Wake pale Mlima wa Mizeituni wangetazamia kuishi mpaka waone kutokea kwa makristo wa uongo na manabii wa uongo ambao wangetenda miujiza mikubwa. Na bila shaka wangetazamia kumwona Yesu akirudi mawinguni kama umeme.
Hatari ya kurudi nyuma wakati huo itakuwa kubwa sana, maana mateso dhidi ya waamini yatakuwa makali mno na makristo wa uongo na manabii wa uongo watashawishi watu sana kutokana na miujiza yao. Hii ndiyo sababu Yesu anarudia tena na tena kuwaonya wanafunzi Wake kuhusu yatakayotokea muda mfupi tu kabla ya kurudi Kwake. Hakutaka wao wapotoshwe kama itakavyokuwa kwa wengi. Waamini wa kweli na walio thabiti watamngoja Yesu arudi mawinguni kama umeme, ambapo wale wasiokuwa wafuasi Wake kweli watavutwa kwa makristo hao wa uongo kama tai wanavyovutiwa na mzoga nyikani.
Ishara Mawinguni
Yesu akaendelea hivi:Lakini mara baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika, ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu (Mathayo 24:29-31).Mifano au picha katika sehemu hii ya mafundisho ya Yesu pale Mlima wa Mizeituni bila shaka ingekuwa inafahamika na Wayahudi wa siku Zake, maana inatoka katika Isaya na Yoeli, na inazungumzia hukumu ya mwisho ya Mungu, mwisho wa dunia. Mara nyingi huitwa “siku ya Bwana”, wakati jua na mwzi vitatiwa giza (ona Isaya 13:10, 11; Yoeli 2:31). Ndipo wakazi wote wa dunia watakapomwona Yesu akirudi mawinguni katika utukufu Wake, nao wataomboleza. Kisha malaika wa Yesu “watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu,” kuonyesha kwamba waamini watanyakuliwa na kukusanywa ili kumlaki Yesu mawinguni, na hayo yote yatatokea baada ya mlio wa “baragumu”.
Hapa tena, kama ungemwuliza Petro, Yakobo au Yohana ikiwa Yesu angewarudia kabla au baada ya wakati wa mpingakristo na dhiki kuu, bila shaka wangesema, “Baada.”
Kurudi Kwake, Na Unyakuo
Hii sehemu ya Mafundisho ya pale Mlima wa Mizeituni inaeleweka sana, kulingana na tukio ambalo Paulo aliandika juu yake, ambalo bila shaka ni Unyakuo wa kanisa, ingawa waandishi wengi wa vitabu vya kufafanua Biblia wanasema linatokea kabla ya kipindi cha Dhiki kuanza. Hebu tazama andiko lifuatalo, tulilotazama mwanzoni mwa sura hii.Lakini ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko,na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tuli hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo. Lakini ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani n salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa (1Wathes. 4:13 – 5:3. Maneno mepesi kukazia).Paulo aliandika juu ya Yesu kuja kutoka mbinguni kwa parapanda ya Mungu na kwamba waamini watanyakuliwa “mawinguni ili kumlaki Bwana hewani.” Ni sawa kabisa na yale Yesu aliyokuwa akieleza katika Mathayo 24:30, 31 – yanayotokea baada ya kutokea kwa mpingakristo na dhiki.
Tena, Paulo alipoendelea kuandika kuhusu kurudi kwa Kristo, anataja kwamba ingetokea lini – “majira na nyakati” – na kuwakumbusha wasomaji wake kwamba walikuwa wanafahamu vizuri sana kwmaba “siku ya Bwana ingekuja kama mwivi anavyokuja usiku.” Paulo aliamini kwamba kurudi kwa Kristo na Unyakuo wa waaminio ungetokea “siku ya Bwana,” siku ambapo hasira kali na maangamizi vingewapata wale waliokuwa wanatazamia “amani na salama.” Kristo anaporudi kulinyakua kanisa Lake, hasira Yake itashuka juu ya dunia.
Hili linakubaliana vizuri sana na kile ambacho Paulo aliandika katika barua kwa Wathesalonike baadaye, kuhusu kurudi kwa Kristo na hasira Yake.
Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi; na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbingunipamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu,na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maagamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake; yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakaifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile, (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu). (2Wathes. 1:6-10. Maneno mepesi kukazia)Paulo alisema kwamba wakati ambao Yesu angerudi kuwapa nafuu Wathesalonike waliokuwa wanateswa (ona 1Wathes. 1:4, 5), angetokea “pamoja na malaika wake katika mwali wa moto” ili kuwaadhibu wale waliokuwa wanawatesa wao, kutoa hukumu ya haki, inayostahili. Hii haifanani na kile kinachosemwa na wengi, kwamba Unyakuo utatokea kabla ya dhiki, na kanisa kunyakuliwa na Kristo kabla ya kile kipindi cha dhiki cha miaka saba kuanza. Hii pia huitwa kuja kwa siri kwa Yesu ili kunyakua kanisa Lake. Hapana kabisa! Maelezo haya yanafanana na kile ambacho Yesu alieleza katika Mathayo 24:30, 31 – kurudi Kwake karibu aumwishoni mwa kipindi cha dhiki kuu – anapowanyakua waaminio na kumimina hasira Yake juu ya wasoiamini.
Siku Ya Bwana
Baadaye, katika barua hiyo hiyo, Paulo aliandika hivi:Basi ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo (2Wathes. 2:1, 2).Kwanza: Ona kwamba mada ya Paulo ni kurudi kwa Kristo na Unyakuo. Aliandika kuhusu “kukusanyika kwetu mbele zake,” akitumia maneno yale yale ambayo Yesu alitumia katika Mathayo 24:31, alipozungumza juu ya malaika ambao “wangekusanya” wateule Wake “kutoka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho ule.”
Pili: Ona kwamba Paulo anayaita matukio hayo kuwa ni “siku ya Bwana,” sawa na alivyofanya katika 1Wathesalonike 4:13 hadi 5:2. Hilo liko wazi kabisa.
Kisha anaendelea hivi:
Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yoyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu (2Wathes. 2:3, 4. Maneno mepesikukazia).Wakristo Wathesalonike walikuwa wanadanganywa kwa namna fulani kwamba siku ya bwana – ambayo kulingana na Paulo lazima ianze kwa Unyakuo na kurudi kwa Kristo – ilikuwa imekwisha fika. Akatamka wazi wazi kwamba haiji mpaka baada ya ule ukengeufu (labda ndiyo kule kurudi nyuma ambako Yesu alizungumzia katika Mathayo 24:10) na baada ya mpingakristo kujitangaza kwamba ni Mungu kutoka hekalu la Yerusalemu. Basi, Paulo anawaambia waamini Wathesalonike wazi wazi kwamba wasitazamie kurudi kwa Kristo – au Unyakuo – wala siku ya Bwana, mpaka baada ya tamko la mpingakristo kwamba ni Mungu.[6]
Kisha, Paulo anaelezea kuhusu kurudi kwa Kristo na jinsi anavyomwangamiza kabisa mpingakristo.
Je, hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo? Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake. Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake; yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa (2Wathes. 2:5-10).Paulo alitamka kwamba mpingakristo atakomeshwa “kwa ufunuo wa kuja Kwake” Kristo. Kama “ufunuo” Wake ni sawa na ule unaotajwa wakati wa Unyakuo – kiasi cha mistari tisa nyuma (ktk 2:1), basi mpingakristo atauawa wakati huo huo ambapo Kanisa litakusanywa ili kumlaki Bwana hewani. Hii inalingana na taarifa itolewayo katika Ufunuo sura ya 19 na 20. Hapo tunasoma juu ya kurudi kwa Kristo (ona Ufunuo 19:11-16), kuangamizwa kwa mpingakristo na majeshi yake (ona 19:17-21), kufungwa kwa Shetani (ona 20:1-3) na “ufufuo wa kwanza” (ona 20:4-6), ambapo waamini waliouawa katika kipindi cha Dhiki yamiaka saba watafufuliwa. Kama huu ndiyo ufufuo wa kwanza kweli kweli kwa maana ya jumla kwamba ni kwa ajili ya wenye haki, basi hakuna mashaka kwamba Unyakuo na kurudi kwa Kristo katika hasira Yake kunatokea wakati huo huo ambapo mpingakristo anaharibiwa, maana, Maandiko yanatuambia wazi kabisa kwamba wote waliokufa katika Kristo watafufuliwa wakati wa Unyakuo (ona 1Wathes. 4:15-17).[7]
Kuwa Tayari
Hebu turudi tena kwenye Mafundisho pale Mlima wa Mizeituni.Basi kwa mtini jifunzeni mfano. Tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu. Nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. Amin nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.[8]Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe (Mathayo 24:32-35).Yesu hakutaka wanafunzi Wake wanaswe bila kufahamu – na hilo ndilo jambo la msingi katika Mafundisho ya pale Mlima wa Mizeituni. Wangejua kwamba “yuko malangoni” baada ya kuona “mambo hayo yote” – dhiki duniani kote, kurudi nyuma kwa watu, kutokea kwa manabii na makristo wa uongo, tangazo la mpingakristo kwamba ni Mungu, na kutiwa giza jua na mwezi pamoja na kuanguka kwa nyota, wakati karibu na kurudi Kwake.
Ila, baada tu ya kuwaambia kuhusu ishara zitakazotangulia kuja Kwake kwa miaka michache, au miezi au siku, aliwaambia sasa wakati hasa wa kurudi Kwake ungebakia kuwa siri.
Walakini kwa habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake (Mathayo 24:36).Mara nyingi andiko hili linatajwa kinyume cha mantiki yake! Kwa kawaida linatajwa ili kuunga mkono dhana kwamba hatuna habari Yesu atarudi lini, kwa sababu anaweza kurudi wakati wowote na kunyakua kanisa. Lakini katika mantiki yake, Yesu hakumaanisha hicho. Alikuwa ndiyo kamaliza kuhakikisha kwamba wanafunzi Wake wangekuwa tayari kwa ajili ya kurudi Kwake kwa kuwaambia ishara nyingi ambazo zingetokea muda mfupi tu kabla ya kurudi Kwake. Sasa anachowaambia ni kwamba, siku hasa na saa havitafunuliwa kwao. Tena, Yesu hasemi juu ya kuja Kwake mara ya kwanza kabla ya kipindi cha Dhiki ya miaka saba kuanza, wakati ambapo kanisa lingenyakuliwa, bali kuhusu kurudi Kwake wakati wa mwisho au karibia mwisho wa Dhiki. Hilo halina matatizo ukitazama mantiki vizuri.
Je, Kurudi Kwake Hakujulikani Kabisa?
Hoja ambayo mara nyingi hutumika dhidi ya Unyakuo kutokea karibu au wakati wa mwisho wa Dhiki ni kwamba kurudi kwa namna hiyo kusingekuwa kitu kisichojulikana kama Yesu alivyodaiwa kusema, kwa sababu kurudi kwa namna hiyo kungetazamiwa kwa matukio ya Dhiki. Lazima kuwe na Unyakuo kabla ya dhiki, la sivyo waamini wasingehitaji kuwa tayari na kukaa macho kama Maandiko yasemavyo wanapaswa kuwa, maana watajua ni miaka saba au zaidi kabla ya Yesu kurudi.Ila, hoja hii inapingwa na ukweli kwamba lengo kuu la Mafundisho ya Yesu pale Mlima wa Mizeituni lilikuwa ni kuhakikisha kwamba wanafunzi Wake wawe tayari kwa ajili ya kurudi Kwake wakati au karibu na mwisho wa Dhiki, naye aliwafunulia ishara nyingi tu ambazo zingetangulia kuja Kwake. Mbona Mafundisho ya Mlimani yamejaa mashauri mengi sana kwamba watu wawe tayari na kuwa macho, ingawa Yesu alijua kwamba kurudi Kwake kuko mbele miaka mingi sana baada ya kusema maneno hayo? Bila shaka ni kwa sababu Yesu aliamini kwamba Wakristo wanahitaji kuwa tayari na kuwa macho hata ingawa kurudi Kwake bado kuko miaka mingi mbele. Mitume ambao katika barua zao waliwashauri waamini kuwa macho na kuwa tayari kwa ajili ya kurudi kwa Yesu walikuwa wanamwiga Yesu Mwenyewe.
Tena, wale wanaoamini kwamba Unyakuo kabla ya dhiki ndiyo wenye kuhalalisha mashauri yoyote ya kuwa tayari, wana tatizo lingine. Kulingana na mawazo yao, kurudi kwa Yesu mara ya kwanza hutangulia dhiki kwa miaka saba. Kwa hiyo, kurudi kwa Yesu mara ya kwanza kulingana na hoja zao hakuwezi kutokea wakati wowote – lazima itakuwa ni miaka saba kabla ya Dhiki kuanza. Basi, hakuna haja ya kutazamia kwamba Yesu atarudi mpaka matukio duniani yakamilike na kuwa tayari kuanza miaka saba ya Dhiki. Matukio hayo yanaweza kutazamiwa na kuhakikishwa kabisa.
Wengi wenye kuamini Unyakuo kabla ya dhiki – kama ni wakweli – watasema kwamba wanajua Yesu hatarudi leo wala kesho kwa sababu ya hali ya kisiasa duniani. Bado yapo matukio yaliyotabiriwa ambayo hayana budi kutimizwa kabla ya ile miaka saba ya Dhiki kuanza. Kwa mfano: Kama tutakavyoona katika kitabu cha Danieli, mpingakristo atafanya agano na Israeli kwa miaka saba, na huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kipindi cha Dhiki. Hivyo basi, kama Unyakuo unatokea miaka saba kabla ya dhiki kuanza, lazima utokee wakati mpingakristo atakapofanya agano lake la miaka saba na Israeli. Basi, hakuna haja ya wale wanaoshikilia kwamba Unyakuo utafanyika kabla ya Dhiki kutazamia Yesu atarudi kabla ya kuona kitu katika siasa kinachofanya hayo yawezekane.
Zaidi ya hayo – kwa wale wanaoamini kwamba Unyakuo utatokea kabla ya dhiki, na kuamini kwamba Yesu atarudi mwishoni mwa Dhiki pia, maana yake ni kwamba siku kamili ya kurudi kwa Yesu mara ya pili inaweza kujulikana kimahesabu. Mara tu Unyakuo utokeapo, mtu yeyote angeweza kukadiria na kujua kile ambacho Yesu alisema ni Baba tu akijuacho. Unachofanya ni kuhesabu mbele miaka saba tu.
Tuseme tena hivi – Kutokana na yale ambayo Yesu alisema, Yeye hakutaka kurudi Kwake kuwe kitu cha kuwashtua watu. Ukweli ni kwamba alitaka kurudi Kwake kutazamiwe, na hivyo akataja matukio kadhaa ya Dhiki. Yesu hakutaka wanafunzi Wake wakutwe hawako tayari, kama ambavyo dunia itakutwa. Basi anaendelea kusema hivi katika Mafundisho Yake pale Mlima wa Mizeituni:
Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile ziliozkuwa kabla ya gharika watu walivyokuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.[9] Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja (Mathayo 24:37-44).Hapa tena, kitu ambacho Yesu anajali ni kwamba wanafunzi Wake wawe tayari kwa ajili ya kurudi Kwake. Hicho ndicho kilisababisha yote aliyosema kabla ya hapa na baada ya hapa, katika mafundisho Yake.Maonyo Yake mwengi kwamba wawe tayari na wakeshe si kwamba ni kwa kuwa kurudi Kwake kutakuwa kwa kushtukiza, bali ni ishara ya jinsi ambavyo itakuwa vigumu kwa sababu ya upinzani wa wakati wenyewe, kuendelea kuwa macho na kuwa tayari. Basi, wale wanaotarajia Unyakuo kabla ya Dhiki, wakati wowote, wanaodhani kwamba wako tayari kuliko Wakristo wengine, wanaweza wasiwe tayari kwa uhalisi kabisa, kwa kile kinachokuja. Kama hawatazamii dhiki yoyote na wajikute katikati ya mateso ya dunia nzima, wakati wa utawala wa mpingakristo, jaribu la kuanguka linaweza kuwazidi nguvu. Afadhali kuwa tayari kwa kile kinachofundishwa na Maandiko kwamba kitatokea.
Halafu tena – kama ungemwuliza Petro, Yakobo au Yohana kwamba walitazamia kumwona lini Yesu akirudi, wangekwambia kuhusu ishara hizo zote ambzo Yesu aliwaambia zingetokea, kabla ya kurudi Kwake.Wasingetazamia kumwona kabla ya kipindi cha dhiki, au kutokea kwa mpingakristo.
Mwivi Usiku
Ona kwamba hata mfano wa Yesu wa “mwivi usiku” uko katika mantiki ya Yeye kudhihirisha ishara nyingi ambazo zingewasaidia wanafunzi Wake wasinaswe ghafula kwa kurudi Kwake. Basi, mfano huo hauwezi kutumiwa kisahihi kuonyesha kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa na wazo lolote kuhusu Yesu anarudi lini.Paulo na Petro walitumia mfano wa Yesu wa “mwivi usiku” walipokuwa wanaandika kuhusu “siku ya Bwana” (ona 1Wathes. 5:2-4; 2Petro 3:10). Waliamini huo mfano ulikuwa na maana kwa habari ya Yesu kurudi kwa ghadhabu wakati wa au mwisho wa Dhiki ya miaka saba. Ila, Paulo aliwaambia hivi wasomaji wake: “Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi” (1Wathes. 5:4). Yeye alitafsiri kwa usahihi mfano wa Yesu, akitambua kwamba wale walio macho na makini kuona zile ishara, na wenye kumfuata Yesu kwa utiifu, hawakuwa gizani mpaka kuja kwa Kristo kuwapate kwa ghafula. Kwa watu namna hiyo, Yesu asingekuja kama mwivi usiku. Ni wale walio gizani tu ndiyo wangeshtushwa – na ndivyo Yesu alivyofundisha. (Ona vile vile matumizi ya Yesu ya maneno “mwivi usiku” katika Ufunuo 3:3 na 16:15. Hapo anatumia maneno hayo kusema juu ya kuja Kwake kwenye vita ya Har-magedoni.)
Kuanzia hapa na kuendelea katika Mafundisho Yake ya pale Mlima wa Mizeituni, Yesu alirudia kuwaonya wanafunzi Wake kuwa tayari kwa ajili ya kurudi Kwake. Hapo hapo akawaambia pia jinsi ya kuwa tayari, aliposema mifano kuhusu mtumwa asiyekuwa mwaminifu, kuhusu wanawali kumi, na kuhusu talanta, na baadaye akatabiri hukumu ya kondoo na mbuzi (yote inafaa kusomwa). Katika hiyo mifano yote, aliwaonya kwamba jehanamu ilikuwa inawasubiri wale wote wasiokuwa tayari kwa ajili ya kurudi Kwake (ona Mathayo 24:50, 51; 25:30, 41-46). Njia ya kuwa tayari ni kupatikana ukifanya mapenzi ya Mungu, wakati Yesu atakaporudi.[10]
Hoja Nyingine
Kuna wanaopinga Unyakuo unaotokea karibu na, au mwisho wa Dhiki kwa msingi kwamba, kulingana na Biblia, wenye haki hawaadhibiwi pamoja na wasio haki. Ushahidi ni mifano ya watu kama Nuhu, Lutu na Waisraeli kule Misri.Kweli, tunazo sababu nzuri tu za kuamini kwamba wenye haki hawatakutwa na ghadhabu ya Mungu wakati wa dhiki ya miaka saba, maana hilo litakuwa kinyume na ahadi nyingi na mifano mingi ya Biblia. (Ona mfano: 1Wathes. 1:9, 10; 5:8).
Lakini, Yesu alitabiri juu ya dhiki kuu ambayo ndani yake wenye haki watateseka. Mateso hayo hayatatoka mikononi mwa Mungu, bali mikononi mwa wasioamini. Wakristo hawaepushwi na mateso – wameahidiwa mateso. Katika kipindi cha Dhiki ya miaka saba, waamini wengi watapoteza maisha yao (ona Mathayo 24:9; Ufunuo 6:9-11; 13:15; 16:5-6; 17:6; 18:24; 19:2). Wengi watakatwa vichwa (ona Ufunuo 20:4).
Basi, kama kila mwamini katika taifa fulani atauawa, hakutakuwa na chochote cha kuzuia ghadhabu ya Mungu isimwangukie kila mmoja katika taifa hilo. Na kwa hakika – kama kuna waamini katika taifa, Mungu aweza kuwalinda kutokana na huku Zake zitakapokuwa zinawaangukia waovu. Wakati wa hukumu Zake kule Misri katika siku za Musa, alithibitisha hilo. Mungu alizuia hata mbwa asibweke kinyume cha Mwisraeli, huku hukumu baada ya nyingine kushuka juu ya Wamisri jirani (ona Kutoka 11:7). Vivyo hivyo tunasoma katika kitabu cha Ufunuo kuhusu nzige wenye kuuma watu, watakaoachiliwa ili kuwatesa waovu wa dunia kwa miezi mitano, lakini wanaambiwa na hawaruhusiwi kuwatesa Wayahudi mia na arobaini na nne elfu (144,000) watakaokuwa wametiwa muhuru maalum kwenye vipaji vya nyuso zao (ona Ufunuo 9:1-11).
Unyakuo Katika Kitabu Cha Ufunuo
Hakuna popote katika Kitabu cha Ufunuo tunaposoma juu ya Unyakuo wa kanisa, wala hatusomi juu ya kutokea kwa Kristo kwingine, isipokuwa katika Ufunuo 19, anapokuja ili kumwua mpingakristo na majeshi yake katika vita ya Har-magedoni. Hakuna lolote linalosemwa kuhusu Unyakuo kutokea hata hapo. Ila, ufufuo wa wafia dini wa Dhiki unatajwa kutokea wakati huo (ona 20:4). Kwa kuwa Paulo aliandika kwamba wafu katika Kristo watafufuliwa wakati wa kurudi kwa Kristo, ambapo pia kanisa litanyakuliwa, mstari huu pamoja na mingine tuliyokwisha tazama, hutuongoza kuamini kwamba Unyakuo hautatokea mpaka mwisho wa Dhiki ya miaka saba, kama inavyoonekana katika Ufunuo 19 na 20. Lakini, yapo mawazo mengine tofauti.Kuna wanaopata Unyakuo katika Ufunuo sura ya 6 na 7. Katika Ufunuo 6:12 na 13, tunasoma juu ya jua kuwa “jeusi kama gunia la singa” na nyota kuanguka kutoka mbinguni – ishara mbili ambazo Yesu alisema zingetokea muda mfupi tu kabla ya kuonekana Kwake na kuwakusanya wateule (ona Mathayo 24:29-31). Kisha baadaye katika sura ya 7, tunasoma juu ya kundi kubwa la watu wakiwa mbinguni, kutoka kila taifa, kabila na lugha, ambao “wametoka katika dhiki ile kuu” (7:14). Hawatajwi kwamba ni wafia dini kama wanavyotajwa wengine katika sura iliyotangulia (ona 6:9-11), na hilo linatufanya tuseme kwamba wamenyakuliwa, hawajauawa – ni waaminio waliokombolewa kutoka katika dhiki ile kuu.
Ni sahihi kudhani kwamba Unyakuo utatokea wakati fulani mara tu baada ya matukio hayo ya mbinguni yanayotajwa katika Ufunuo 6:12 na 13, kwa sababu yanafanana na yale aliyosema Yesu katika Mathayo 24:29-31. Ila, hatuna ishara iliyo dhahiri kuhusu wakati wa kutokea hayo mambo yanayotajwa katika Ufunuo 6:12 na 13, katika kipindi cha dhiki ya miaka saba. Kama matukio yanayotajwa katika Ufunuo 6:1-13 yanafuatana, na kama Unyakuo unatokea mara tu baada ya 6:13, hilo linatuongoza kuamini kwamba Unyakuo hautatokea mpaka baada ya kufunuliwa kwa mpingakristo (ona 6:1, 2), na vita ya dunia nzima (ona 6:3-4), njaa (ona 6:5, 6), kufa kwa robo ya watu wa duniani kwa vita, njaa, magonjwa na wanyama wakali (ona Ufunuo 6:7-8), na wafia dini wengi kupatikana (ona Ufunuo 6:9-11). Hakika matukio hayo yote yanayotajwa yanaweza kutokea kabla ya kumalizika kipindi cha Dhiki cha miaka saba, lakini pia yanaweza kuwa ndiyo yatakayotokea katika kipindi chote cha miaka saba cha dhiki, na Unyakuo kuwa mwisho kabisa.
Wazo la Unyakuo kutokea kabla ya mwisho wa miaka saba ya dhiki linaongezewa uzito na kweli kwamba Kitabu cha Ufunuo kinaeleza juu ya makundi mawili ya hukumu saba, baada ya Ufunuo sura ya 8, kama ifuatavyo: “hukumu za baragumu” na “hukumu za vitasa”. Hizi za vitasa zinasemekana ndiyo mwisho wa ghadhabu ya Mungu (ona 15:1). Lakini, kabla ya hukumu hizo za vitasa kuanza, Yohana anawaona “wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, wamesimama kandokando ya hiyo bahari ya kioo” (15:2). Hawa watakatifu washindi yawezekana walinyakuliwa. Lakini tena, yawezekana walifia imani yao. Maandiko hayaelezi. Tena, hatujui kama mambo ya 15:2 yana uhusiano wowote na maelezo ya mambo yanayotajwa hapo.
Kweli nyingine inayopatikana katika Ufunuo, yenye kuweza kuongezea uzito kwenye wazo la Unyakuo kutokea kabla ya mwisho wa miaka saba, ni hili: Wakati wa “hukumu ya baragumu” ya tano katika Ufunuo 9:1-12, tunaambiwa kwamba nzige wenye kuuma wataruhusiwa kuwadhuru wale tu “wasiokuwa na muhuri ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao” (9:4). Watu pekee tunaoambiwa watakuwa na muhuri ni Waisraeli mia na arobaini na nne elfu (144,000) tu (ona Ufunuo 7:3-8). Basi inaonekana kwamba waamini wengine wote itabidi wanyakuliwe kabla ya baragumu hiyo ya tano ya hukumu; vinginevyo, hawataepuka nguvu za hao nzige waumao. Tena, kwa sababu nzige hao watawaumiza watu kwa miezi mitano (9:5, 10), inadhaniwa kwamba ni lazima Unyakuo utokee miezi mitano kabla ya kumalizika kwa miaka ile saba ya Dhiki.
Kuna jinsi ya kufafanua hoja hizo. Pengine kuna wengine waliotiwa muhuru ambao hawatajwi katika kitabu cha Ufunuo. Vyovyote vile, kama hili linathibitisha kwamba Unyakuo utatokea kabla ya hukumu yabaragumu ya tano, pia linaonyesha kwamba kuna kundi moja la waamini ambao hawatanyakuliwa kabla ya kuachiwa kwa hao nzige waumao – wale Waisraeli mia na arobaini na nne elfu (144,000) waliotiwa muhuri. Ila, watakuwa na alama ya kuwalinda wasipatikane na ghadhabu ya Mungu, itakayokuwa inatolewa kwa njia ya nzige hao waumao.
Tuhitimishe. Cha kusema ni kwamba bila shaka Unyakuo utatokea karibu na mwisho au mwishoni kabisa mwa ile miaka saba ya Dhiki. Waamini wasihofu kuhusu ghadhabu ya Mungu, lakini pia wawe tayari kwa ajili ya mateso makali na hata kufa kwa ajili ya imani yao.
Kipindi Cha Dhiki
Hebu tutazame kwa karibu zaidi kile ambacho Maandiko yanafundisha kuhusu ile miaka saba ya Dhiki. Tunapataje saba kwamba ndiyo urefu wa Dhiki? Ni lazima tujifunze kitabu cha Danieli, ambacho kinatoa ufunuo mpana zaidi kuhusu nyakati za mwisho, pamoja na kitabu cha Ufunuo.Katika sura ya tisa ya kitabu chake, tunagundua kwamba Danieli ni mtumwa huko Babeli, na Wayahudi wenzake. Akiwa katika kujifunza kitabu cha Yeremia, Danieli aligundua kwamba muda wa utumwa wa Wayahudi huko Babeli ungekuwa miaka sabini (ona Danieli 9:2; Yeremia 25:11, 12). Baada ya kutambua kwamba kipindi cha miaka ile sabini kinakaribia kumaliziika, alianza kuomba, akitubu dhambi za watu wake na kuomba rehema. Malaika Gabrieli alimtokea kama jibu la maombi yake, na kumfunulia wakati ujao wa taifa la Israeli, mpaka wakati wa Dhiki na kurudi kwa Kristo. Unabii ulio katika Danieli 9:24-27 ni wa kushangaza sana katika Maandiko. Unabii wenyewe ni kama ifuatavyo, pamoja na maelezo zaidi katika mabano.
Muda wa majuma sabini [bila shaka ni majuma yanayowakilisha miaka kama tutakavyoona – jumla ya miaka 490] umeamriwa juu ya watu wako [Israeli], na juu ya mji wako mtakatifu [Yerusalemu], ili kukomesha makosa [labda maana yake ni tendo kuu la dhambi kwa Israeli – kumsulubisha Masiya wao], na kuishiliza dhambi [pengine maana yake ni kazi ya ukombozi ya Kristo pale msalabani], na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu [maana yake ni ile kazi ya Kristo ya ukombozi pale msalabani], na kuleta haki ya milele [mwanzo wa utawala wa Yesu duniani], na kutia muhuri maono na unabii [pengine kuonyesha mwisho wa kuandikwa kwa Maandiko Matakatifu, au kutimizwa kwa unabii wote unaohusiana na utawala wa Miaka elfu], na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu [pengine kusimamishwa kwa hekalu la kipindi cha utawala wa Kristo miaka elfu moja hapa duniani]. Basi ujue na kufahamu ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu [amri hii ilitolewa na Mfalme Artashasta mwaka wa 445 K.K.] hata zamani zake masihi aliye mkuu [Bwana Yesu Kristo]; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili [yaani, jumla ya majuma 69 au miaka 483] utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu [hii inahusu kujengwa upya kwa Yerusalemu, uliokuwa umeharibiwa na WaBabeli]. Na baada ya yale majuma sitini na mawili [yaani, miaka 483 baada ya amri ya mwaka wa 445 K.K.], masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu [Yesu angesulubiwa mwaka wa 32B.K., tukihesabu mwaka kulingana na kalenda ya Kiyahudi yenye siku 360 kwa mwaka]; na watu [Warumi] wa mkuu atakayekuja [mpingakristo] watauangamiza mji na patakatifu [maelezo kuhusu kuharibiwa kwa Yerusalemu mwaka wa 70 B.K. na majeshi ya Kirumi chini ya uongozi wa Tito]; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa. Naye [huyo ‘mkuu atakayekuja’ – mpingakristo] atafanya agano thabiti na watu wengi [Israeli] kwa muda wa juma moja [au miaka saba – hiki ni kipindi cha Dhiki]; na kwa nusu ya juma hiyo [yaani, miaka mitatu na nusu] ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu [wakati mpingakristo atakapojisimamisha mwenyewe katika hekalu la Kiyahudi huko Yerusalemu na kujiita Mungu – ona 2Wathes. 2:1-4]; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu [Yesu atakuja, na kumshinda mpingakristo] (Danieli 9:24-27. Maneno mepesi kukazia).
Miaka 490 Maalum
Baada ya amri ya mwaka wa 445 K.K. iliyotolewa na Mfalme Artashasta kwamba Yerusalemu ujengwe tena, Mungu alitoa miaka 490 maalum sana katika historia ya wakati ujao. Lakini hiyo miaka haikuwa yenye kufuatana – iligawanywa katika sehemu mbili – moja yenye miaka 483 na nyingine yenye miaka saba. Wakati ile miaka 483 ya kwanza ilipokamilika (mwaka ule Yesu aliposulubiwa), saa ilisimama. Danieli asingeweza kudhani kwamba saa ingesimama kwa muda unaozidi miaka elfu mbili! Wakati fulani huko baadaye, saa itaanza tena kutembea, na itatembea kwa miaka saba ya mwisho. Hiyo miaka saba ya mwisho haiitwi tu “Dhiki”, bali pia inajulikana kama “juma la sabini la Danieli.”Hiyo miaka saba imegawanywa katika vipindi viwili vya miaka mitatu na nusu. Kama tulivyojifunza katika unabii wa Danieli, itakapofikia katikati, mpingakristo atavunja agano lake na Israeli na “kukomesha sadaka na dhabihu.” Kisha, kama alivyotuambia Paulo, ataketi katika hekalu la Yerusalemu na kujitangaza kuwa ni Mungu.[11] Hilo ndilo “chukizo la uharibifu” alilotaja Yesu (ona Mathayo 24:15). Ndiyo sababu waamini wa Uyahudi wanapaswa “kukimbilia milimani” (Mathayo 24:16), maana huo ndiyo mwanzo wa dhiki mbaya zaidi iliyowahi kuowepo duniani (ona Mathayo 24:21).
Yawezekana “kukimbia kwa Wayahudi” kulionekana na Yohana kwa jinsi ya mfano katika maono yake, katika sura ya 12 ya kitabu cha Ufunuo. Kama ndivyo, waamini wa Kiyahudi watakuta mahali maalum pa usalama pameandaliwa kwa ajili yao huko nyikani, watakapo”tunzwa na kulishwa” kwa miaka mitatu na nusu, ambao ndiyo muda utakaokuwa umebaki wa kipindi cha Dhiki ya miaka saba (ona Ufunuo 12:6, 13-17). Yohana aliona Shtani akikasirishwa na kutoroka kwao, na vita iliyofuata aliyoifanya kwa wale wengine “wazishikao amri za Mungu na ushuhuda wa Yesu” (Ufunuo 12:17). Ndiyo sababu ni vizuri waamini duniani kote wakimbilie usalama katika maeneo yaliyofichika, wakati mpingakristo atakapotangaza ‘uungu’ wake huko Yerusalemu.
Ufunuo Wa Mwisho Wa Danieli
Fungu lingine la maandiko lenye kuvutia kutoka Danieli ambalo hatujalitazama, ni ile mistari 13 ya mwisho ya kitabu chake cha kushangaza sana. Ni maneno yaliyotamkwa na malaika. Yanafuata sasa, pamoja na maelezo zaidi katika mabano.Wakati huo Mikaeli [malaika] atasimama, jemadari mkuu asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo [bila shaka hii ni ile dhiki ambayo Yesu alisema juu yake katika Mathayo 24:21]; na wakati huo watu wako wataokolewa [pengine ndiyo kule kukimbia kwa Wayahudi, au kuokolewa kwa waamini wakati wa Unyakuo]; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile. Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele [huu ni ufufuo wa wenye haki na waovu]. Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele. [Baada ya ufufuo wao, wenye hai watapokea miili mipya itakayong’aa kwa utukufu wa Mungu.] Lakini wewe, Ee Danieli, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka. [Maendeleo ya kushangaza sana katika usafirishaji na maarifa katika karne iliyopita yanaonekana kutimiza unabii huu.]
Ndipo mimi, Danieli, nikatazama, na kumbe, wamesimama wengine wawili, mmoja ukingoni mwa mto upande huu, na mmoja ukingoni mwa mto upande wa pili. Na mmoja akamwuliza yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto; ‘Je! Itakuwa muda wa miaka mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu?’ Nami nikamsikia yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji yam to, hapo alipoinua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kueloekea mbinguni; akaapa kwa yeye aliye hai milele na milele, ya kwamba itakuwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati [sawa na miaka mitatu na nusu, kulingana na ufunuo wenye kufumbua katika Ufunuo 12:6 na 12:14); tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mambo hayo yote yatakapotimizwa. [Sawa tu na jinsi Danieli 7:25 ilivyotueleza kwamba watakatifu watatiwa mikononi mwa mpingakristo kwa miaka mitatu na nusu. Inaonekana dhahiri kwamba ni ile miaka mitatu na nusu ya mwisho katika ile miaka saba ya Dhiki. Mwisho wa matukio hayo yote yaliyotajwa na malaika utakuja wakati “nguvu za watakatifu” zitakapokwisha “kuvunjwa.”] Nami nikasikia, lakini sikuelewa; ndipo nikasema, ‘Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje?’ Akasema, ‘Enenda zako, Danieli; maana maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho. Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika [kwa njia ya dhiki bila shaka]; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndiyo watakaoelewa. Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini. [Hizo siku zisitafsiriwe kumaanisha muda utakaopita katikati ya hayo matukio mawili, kwa sababu yote yanatokea katikati ya ile miaka saba. Inatakiwa kueleweka hivi: tangu wakati wa matukio hayo mawili, siku 1,290 zitapitampaka kitu kingine kikubwa kitakapotokea mwishoni. Siku 1290 ni zaidi ya miaka mitatu na nusu kwa siku 30, kwa hesabu ya miaka yenye siku 360. Muda huu hutajwa mara kwa mara katika maandiko ya kinabii ya Danieli na Ufunuo. Sababu ya kuongezwa hizo siku thelathini haitajwi na haijulikani. Tena, malaika akamwambia Danieli hivi:] Heri angojaye, na kuzifikilia siku hizo elfu na mia tatu na thelathini na tano. [Sasa tena tuna siku zingine arobaini na tano zisizojulikana ni za nini.] Lakini enenda zako hata utakapokuwa mwisho ule; maana wewe utastarehe, nawe utasimama [kufufuka kwa Danieli mwenyewe] katika kura yako mwisho wa siku hizo. (Danieli 12:1-13).Ni dhahiri kwamba kitu kizuri sana kitatokea mwisho wa hizo siku 75 za ziada! Itabidi tusubiri ili tuone.
Kutokana na kusoma sura za mwisho za kitabu cha Ufunuo, tunajua kuna matukio mengi ambayo yatakuwepo mara tu baada ya Kristo kurudi – moja likiwa Karamu ya Arusi ya Mwana Kondoo. Malaika alimwambia Yohana hivi juu ya jambo hilo, “Heri walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo” (Ufunuo 19:9). Pengine hii ndiyo baraka hiyo hiyo inayotajwa na malaika aliyesema na Danieli. Kama ni hivyo, karamu hiyo ya utukufu mwingi itatokea kama miezi miwilina nusu hivi baada ya kurudi kwa Yesu.
Labda zile siku sabini na tano zimejaa vitu vingine ambavyo tunajua vitatokea, kulingana na ilivyoandikwa katika sura za mwisho za kitabu cha Ufunuo, kama vile kutupwa kwa mpingakristo na nabii wa uongo katika ziwa la moto; kufungwa kwa Shetani; na kuanzishwa kwa utawala wa ufalme wa Kristo duniani kote (ona Ufunuo 19:20 hadi 20:4).
Kipindi Cha Miaka Elfu
Utawala wa Miaka Elfu ni jina linaloeleza wakati ambapo Yesu Mwenyewe atatawala dunia nzima kwa kipindi cha miaka elfu moja (ona Ufunuo 20:3, 5, 7). Hii inatokea baada ya ile Dhiki ya miaka saba. Isaya aliona utawala wa Kristo juu ya dunia, miaka elfu tatu na zaidi iliyopita. Anaeleza hivi:Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa … Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani hayatakuwa na mwisho kamwe, katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake, kuuthibitisha na kuutegemeza kwa hukumu na kwa haki, tangu sasa na hata milele (Isaya 9:6, 7. Manenomepesi kukazia).Vivyo hivyo, malaika Gabrieli alimtangazia Mariamu kwamba Mtoto wake angetawala ufalme usio na mwisho. Alimwambia hivi:
Malaika akamwambia, ‘Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho’ (Luka 1:30-33. Maneno mepesi kukazia).[12]Wakati wa Miaka Elfu, Yesu binafsi atatawala kutoka Yerusalemu, pale Mlima Sayuni, na mlima huo utainuliwa na kuwa mrefu kuliko sasa. Utaala Wake utakuwa wa haki kabisa kwa mataifa yote, na itakuwepo amani kamili na halisi duniani kote.
Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, ‘Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake. Maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upana juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe (Isaya 2:2-4).Hata Zekaria naye alitabiri hayo hayo, kama ifuatavyo:
BWANA wa majeshi asema hivi, ‘Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu.’ BWANA asema hivi, ‘Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa BWANA wa majeshi utaitwa, Mlima Mtakatifu.’ … BWANA wa majeshi asema hivi, ‘Itatokea halafu ya kwamba watakuja mataifa na wenyeji wa miji mingi; wenyeji wa mji huu watauendea mji huu, wakisema, ‘Haya! Twendeni zetu kwa haraka tuombe fadhili za BWANA, na kumtafuta BWANA wa majeshi; mimi nami nitakwenda.’ Naam, watu wa kabila nyingi na mataifa hodari watakuja Yerusalemu kumtafuta BWANA wa majeshi, na kuomba fadhili za BWANA. BWANA wa majeshi asema hivi, ‘Siku hizo watu kumi, wa lugha zote za mataifa, wataushika upindo wa nguo yake yeye aliye Myahudi; naama, wataushika wakisema, Tutakwenda pamoja nanyi, kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi’. (Zekaria 8:2-3; 20-23).Biblia inafundisha kwamba waamini watatawala pamoja na Kristo katika kipindi hicho cha miaka elfu moja. Viwango vya majukumu na wajibu zao katika ufalme Wake vitategemeana na uaminifu wao kwa sasa (ona Danieli 7:27; Luka 19:12-27; 1Wakor. 6:1-3; Ufunuo 2:26, 27; 5:9, 10 na 22:3-5).
Tutakuwa katika miili yetu ya ufufuo, lakini watakuwepo watu wengine wakiishi katika miili yao ya kawaida tu duniani. Tena, inaonekana urefu wa maisha utarudishwa, na wanyama wakali watakoma kuwa hivyo.
Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. … Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng’ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema BWANA (Isaya 65:19, 20, 25. Ona pia Isaya 11:6-9).Biblia imetaja sana habari za Miaka Elfu inayokuja – hasa katika Agano la Kale. Ukitaka kujifunza zaidi, soma Isaya 11:6-16; 25:1-12; 35:1-10; Yeremia 23:1-5; Yoeli 2:30 hadi 3:21; Amosi 9:11-15; Mika 4:1-7; Sefania 3:14-20; Zekaria 14:9-21 na Ufunuo 20:1-6.
Vile vile, Zaburi nyingi za kinabii zinahusiana na kipindi cha Miaka Elfu. Kwa mfano: Soma fungu hili katika Zaburi ya 48.
Bwana ndiye aliye mkuu, na mwenye kusifiwa sana. Katika mji wa Mungu wetu, katika mlima wake mtakatifu. Kuinuka kwake ni mzuri sana, ni furaha ya dunia yote. Mlima Sayuni pande za kaskazini, Mji wa Mfalme mkuu. Mungu katika majumba yake amejijulisha kuwa ngome.Maana, tazama, wafalme walikusanyika; walipita wote pamoja. Waliona, mara wakashangaa; wakafadhaika na kukimbia. Papo hapo tetemeko liliwashika, utungu kama wa mwanamke azaaye (Zaburi 48:1-6. Maneno mepesi kukazia).Wakati Yesu atakaposimamisha utawala Wake huko Yerusalemu wakati wa kuanza kwa kipindi cha Miaka Elfu Moja, inaonekana kwamba watawala wengi wa dunia watakaopona Dhiki watapata taarifa ya utawala wa Yesu na kusafiri kwenda huko ili kujionea wenyewe! Watakachokiona kitawashangaza.[13]
Ukitaka Zaburi zingine zenye kusimulia habari za utawala wa Kristo katika Miaka Elfu, angalia Zaburi 2:1-12; 24:1-10; 47:1-9; 66:1-7; 68:15-17; 99:1-9 na 100:1-5.
Umilele
Mwisho wa kipindi cha Miaka Elfu ni mwanzo wa kitu kinachoita na wasomi wa Biblia “umilele”, muda unaoanza kwa mbingu mpya na nchi mpya. Kisha, Yesu atamrudishia Baba kila kitu, kulingana na 1Wakorintho 15:24-28.Hapo ndipo mwisho, [Yesu] atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. Kwa kuwa, ‘Alivitiisha vitu vyote chini ya miguu yake’ [Zaburi 8:6]. Lakini atakaposema, ‘Vyote vimetiishwa,’ ni dhahiri ya kuwa yeye [Baba] aliyemtiishia vitu vyote hayumo. Basi, vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake [Baba], ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote.Shetani ambaye atakuwa amefungwa kwa kipindi chote hicho cha miaka elfu, atafunguliwa mwisho wake. Ndipo atawadanganya wale ambao ndani yao wanamwasi Yesu, waliokuwa wanajifanya kumtii wakati wa kipindi hicho chote (ona Zaburi 66:3).
Mungu atamruhusu Shetani kuwadanganya ili kudhihirisha hali halisi yamiyo yao, waweze kuhukumiwa kihalali. Katika kudanganywa kwao, watajikusanya ili kuushambulia mji mtakatifu – Yerusalemu – lengo lao likiwa kuipindua serikali ya Yesu. Vita haitadumu sana kwa sababu moto utashuka kutoka mbinguni na kuteketeza majeshi yaliyouzunguka mji, na Shetani atatupwa milele katika ziwa la moto na kiberiti (ona Ufunuo 20:7-10).
Kujikusanya huko kwa ajili ya vita kunatabiriwa katika Zaburi ya 2, kama ifuatavyo:
Mbona mataifa wanafanya ghasia, na makabila wanatafakari ubatili? Wafalme wa dunia wanajipanga, na wakuu wanafanya shauri pamoja, juu ya BWANA, na juu ya masihi wake [Kristo], ‘Na tuvipasue vifungo vyao, na kuzitupia mbali nasi kamba zao!’ Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka. Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake. ‘Nami nimemweka mfalme wangu juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.’ [Yesu sasa anazungumza na kusema hivi:] ‘Nitaihubiri amri. BWANA aliniambia, Ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa. Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, na miisho ya dunia kuwa milki yako. Utawaponda kwa fimbo ya chuma, na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi.’ Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili, enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe. Mtumikieni BWANA kwa kicho, shangilieni kwa kutetemeka. Shikeni yaliyo bora, asije akafanya hasira nanyi mkapotea njiani, kwa kuwa hasira yake itawaka upesi. Heri wote wanaomkimbilia!
Hukumu Ya Mwisho
Kabla ya kuanza Umilele, hukumu moja itatolewa. Wasio haki wote wa nyakati zote watafufuliwa kutoka wafu ili wasimame mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na kuhukumiwa kulingana na matendo yao (ona Ufunuo 20:5; 11-15). Kila mtu ambaye kwa sasa yuko Hades (kuzimu) atafikishwa hukumuni hapo. Hukumu hii inajulikana kama “Hukumu ya Kiti Kikubwa cha Enzi, Cheupe”. Kisha, atatupwa Jehanamu – katika ziwa la moto. Hiyo inaitwa “mauti ya pili” (Ufunuo 20:14).Umilele unaanza kwa kupita kwa mbingu na nchi za kwanza, na hivyo kutimiza ahadi ya Yesu ya zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita: “Mbingu na nchi zitapita, bali maneno yangu hayatapita kamwe” (Mathayo 24:35).
Kisha, Mungu ataumba mbingu na nchi mpya, sawa na Petro alivyotabiri katika barua yake ya pili, hivi:
Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi. Katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake (2Petro 3:10-14. Ona pia Isaya 65:17, 18).Hatimaye – Yerusalemu mpya utashuka kutoka mbinguni mpaka chini duniani (ona Ufunuo 21:1, 2). Mawazo yetu hayawezi hata kuanza kuelewa utukufu wa mji huo, wenye eneo kubwa sana – karibu nusu ya bara la Afrika (ona Ufunuo 21:16), au maajabu ya miaka hiyo isiyo na mwisho. Tutaishi katika jamii kamilifu milele, chini ya utawala wa Mungu, kwa utukufu wa Yesu Kristo!
[1] Maandiko mengine yenye kuonyesha imani ya Paulo kwamba Yesu angeweza kurudi katika wakati wa uhai wake ni Wafilipi 3:20; 1Wathes. 3:13; 5:23; 2Wathes. 2:1-5; 1Timo. 6:14, 15; Tito 2:11-13; Waebrania 9:28.
[2] Maandiko mengine yenye kuonyesha imani ya Petro kwamba Yesu angeweza kurudi wakati wa uhai wake ni 2Petro 1:15-19; 3:3-15.
[3] Katika Marko 13:3 wanatajwa wale wanne waliokuwepo: Petro, Yakobo, Yohana na Andrea. Mafundisho ya pale Mlima wa Mizeituni yanapatikanapia katika Marko 13:1-37 na Luka 21:5-36. Utapata habari kama hizo katika Luka 17:22-37 pia.
[4] Mara nyingi ahadi hii huondolewa mahali pake. Watu husema mara kwa mara kwamba kabla Yesu hajarudi, imetupasa kukamilisha kazi ya kuufikia ulimwengu kwa Injili. Lakini, katika mantiki hii, ahadi hii inazungumzia kutangazwa kwa mwisho wa Injili duniani kote kabla ya mwisho wa dunia.
[5] Kama Unyakuo wa kanisa unatokea wakati huo katika ile Dhiki ya miaka saba kama wengine wanavyosema, maagizo ya Yesu kamba waamini wakimbie kuokoa maisha yao yasingekuwa na maana kwa sababu si watanyakuliwa wote?
[6] Hii inapinga hoja kwamba maneno ya Yesu katika Mafundisho pale Mlima wa Mizeituni yanawahusu waamini wa Kiyahudi tu ambao wataokolewa wakati wa Dhiki, maana wengine wote walio-okoka kabla ya Dhiki watakuwa wamekwisha nyakuliwa. Paulo anawaambia waamini Wathesalonike – mataifa – kwamba Unyakuo wao na kurudi kwa Kristo visingetokea mpaka baada ya mpingakristo kujitangaza kwamba ni Mungu, kitu kinachotokea katikati ya Dhiki ya miaka saba.
[7] Kuna wanaosema kwamba huu ufufuo unaotajwa katika Ufunuo 20:4-6 ni sehemu ya pili ya ufufuo wa kwanza, ufufuo uliotokea wakati wa kurudi mara ya kwanza kwa Kristo wakati wa Unyakuo. Nini sababu ya tafsiri hiyo? Kama ufufuo wa Ufunuo 20:4-6 ni wa pili, mbona usiitwe “ufufuo wa pili”?
[8] Ingawa waliomsikia Yesu siku hiyo wanaweza kuwa walidhani kwamba kizazi chao ndicho kingeyaona hayo yote, tunajua sivyo. Basi, lazima tutafsiri maneno ya Yesu katika 24:34 kumaanisha kwamba mambo hayo yote yatafanyika katika kizazi kimoja, au pengine kwamba taifa la Wakristo (au Wayahudi basi) lisingepita mpaka mambo hayo yote yatimie.
[9] Hakuna tofauti yoyote ikiwa mwenye kupatikana na hukumu katika mifano hii ni mwenye kutwaliwa au mwenye kubaki, kama ambavyo watu wengi hubishana. Hoja ni kwamba, kuna watakaokuwa tayari kwa ajili ya kurudi kwa Kristo, na kuna ambao hawatakuwa tayari. Utayari wao utaamua umilele wao.
[10] Ni dhahiri kwamba uwezekano wa wanafunzi wa Yesu kutokuwa tayari wakati wa kurudi Kwake ulikuwepo, maana aliwaonya sana kuhusu hilo. Kama aliwaambia kwamba adhabu ni hukumu ya milele kwa kutokuwa tayari kwa sababu ya dhambi, basi ilikuwa inawezekana kwao kupoteza wokovu kwa sababu ya dhambi. Hili linapaswa kutupa angalizo juu ya umuhimu wa utakatifu, na tutambue kwamba ni upuuzi kusema kwamba waamini hawawezi kupoteza wokovu wao, kama wengine wanavyosema na kufundisha.
[11] Hii inatuonyesha kwamba lazima hekalu la Yerusalemu lijengwe tena maana kwa sasa hakuna hekalu lolote huko Yerusalemu (mwaka 2005 kitabu hiki kinapoandaliwa).
[12] Andiko hili linaonyesha jinsi ilivyo rahisi kukosea kuhusu matukio ya kinabii kwa kusoma isivyo. Mariamu angeweza kudhani kihalali kabisa kwamba Mtoto wake maalum sana angekalia kiti cha enzi cha Daudi baada ya miaka kadhaa. Gabrieli alimwambia angezaa mwana ambaye angetawala juu ya nyumba ya Yakobo, kana kwamba kuzaliwa kwa Yesu na kutawala vingekuwa vitu vinavyofuatana. Mariamu asingeweza kudhani kwamba kuna zaidi ya miaka elfu mbili kati ya kuzaliwa na kutawala. Sisi pia tunapaswa kuwa makini – tusije tukatafsiri unabii vibaya.
[13] Kutokana na maandiko mengine, inaonekana kwamba kipindi cha Miaka Elfu kitaanza kwa wasioamini kujaza dunia, si waamini tu. (Ona Isaya 2:1-5; 60:1-5; Danieli 7:13, 14).