HAMJUI NI ROHO YA NAMNA GANI MLIYO NAYO
(Luka 9:55).
Waumini wanaweza kukosa sana! Vipi? Yanaanza na mawazo hayo, “Mimi ni mwanafunzi wa Bwana. Mimi nipo upande wa Mungu. Kwa hiyo, Mungu yupo upande wangu.” Sasa hii ni hatari! Bila kufikiri sana tunaamini tunayo haki katika tunalosema na tunalotenda kwa sababu tunafikiri eti, ‘Mungu yuko upande wangu. Mimi ninamwakilisha Bwana juu ya maadui Yake ’! Wasamaria hawakumkaribisha Yesu aliposafiri kwenda Yerusalemu, na “wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, ‘Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize.’ ” Unaona? Walifikiri ‘mimi nipo upande wa haki, kwa hiyo ninayo haki katika nitakalotaka kufanya!’ Walifikiri ni sawa wawaangamize watu wale! Lakini Bwana Yesu aliwakemea, “Akawageukia, akawakanya. Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.” Wanafunzi hao walikosa sana. Walifikiri wao ni wawakilishi wa haki ya Bwana, wa ukweli wa Injili kwa wengine. Kinyume chake, walijiruhusu kupatwa na kiburi tu! Kwa urahisi waumini wengine wanaweza kuwashambulia watu, kuwakashifu, kuwashutumu na kutumia lugha ya matusi kwa sababu, eti, haki iko upande wetu, tunatetea kwa ajili ya Bwana na ukweli Wake! Unaweza kuona hiyo kwenye mtandao (hata kwenye Facebook na hasa kwenye ‘Jamiiforums’). ‘Wakristo’ na watu wa dini wanatukanana vibaya sana kwa sababu wanafikiri wapo wawakilishi wa ukweli na haki! Jambo la kushangaa. Wanaacha tabia na roho ya Bwana Yesu kabisa wakati wanafikiri wapo mabalozi ya Bwana! Kuwa ‘mabalozi’ ya Bwana au ‘mwakilishi’ wake, lazima tuwe na tabia yake na kuonyesha tabia yake.
Labda unalosema ni sawa. Lakini BADO haitoshi kama unalosema ni sawa! Haitoshi ‘kuwa na haki’! (It is not engough ‘to be right’). Bali tunapaswa kuwa na tabia ya haki, ya adili (We need to have the right ‘being’). Tunapaswa tuonyeshe na tuwe na tabia ya Bwana, ya upole, ya uvumulivu, ya neema, ya rehema, ya huruma, ya upendo katika ya maisha yetu ya kila siku. “Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu…Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye.” (Wakol.4:6; 2 Tim.2:24,25).
Nilisimulia hadithi ifuatyo katika kanisa moja kijijini: Watu wawili walikuwa wanasafiri na walifika Morogoro. Bwana Upole alianza mazungumzo na Bwana Majivuno:
Bwana Upole: ‘Nafikiri tumefika Iringa, rafiki yangu.’
Bwana Majivuno: ‘Wewe unakosa sana! Mimi najua vizuri sana kuliko wewe! Mji huo siyo Iringa, ni Morogoro.’
Bwana Upole: ‘Labda nimekosea, lakini nafikiri ni Iringa.’
Bwana Majivuno: ‘Labda? Je, hukusikia nililolikuambia? Tupo Morogoro! Mjinga wewe!’
Bwana Upole: ‘Inawezekana rafiki yangu, lakini inaonekana kwangu kuwa ni Iringa.’
Bwana Majivuno: ‘Kwa nini unanipinga? Mimi nimewahi kufika Morogoro. Najua zaidi kuliko wewe! Nyamaza kimya tu!’
Sasa Bwana Majivuno alikasirika sana akaanza kumpiga Bwana Upole kiasi cha kumjeruhi.
Sasa je, nani aliyekuwa na haki? Nani kati yao alisema sawa? Unaona? Bwana Upole hakukosa kwa tabia yake wala kwa maneno yake! Bali kauli yake juu ya mji waliopo haikuwa sawa. Hiyo tu! Bwana
Majivuno alisema iliyo sawa lakini maneno yake na tabia yake haikuwa sawa! Alijiaibisha tu! Yupo ndiye aliyechukua ushindi? Ni wazi – Mwenye upole! Na sisi tunaweza kujiaibisha wenyewe na kuuaibisha ule Ukweli tunaoutetea! Katika kanisa lile ambapo nilisimulia hadithi hiyo alikuwepo mzee wa kanisa mmoja na ilikuwa wazi kwangu haikuwa mtu wa kiroho. Muda mfupi tu baada ya kufundisha pale, mzee yule na mkulima mmoja walibishana juu ya shamba fulani. Yule mzee alikasirika akampiga mkulima kupita kiasi na yule mzee akatoroka! Sikusimulia hadithi ile kwa ajili ya mzee yule, lakini nashangaa neema ya Mungu kwake, yaani, Bwana alitaka kumonyesha kosa la tabia yake na kumwonya juu ya tabia hiyo ili ageuze na asiifanye dhambi.
Nilikuwa pamoja na mchungaji fulani mjini. Alijua Biblia vizuri sana. Lakini tulipokuwepo sokoni alianza kuongea na wauzaji paruparu. Nilishangaa. Inakuwaje tunaweza kuonekana mtu mzuri kanisani lakini kuwa paruparu kwa wengine, kana kwamba wao hawafai kwani ni wasioamini tu? Yakobo anatuonya, “Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.” (Yak.3:10). Kama vile Yakobo na Yohana walivyojiruhusu kuwa wakali kwa wengine kwa sababu walifikiri wao wapo upande wa Mungu, vivyo hivyo wakristo wanaweza kukosa kwa namna hiyo na kujiruhusu kuwadharau na kuwashifu wengine – na kumwaibisha jina la Bwana – kwa sababu wanafikiri, eti, Mungu yupo upande wangu, nimejiunga na timu ishindayo kila mara!
Najua Injili yenyewe inaweza kuwachukiza watu lakini siongei juu ya tabia ya Injili bali tabia yetu tunapozungumza na watu, hasa kuhusu Injili.
Je, unajua ni roho ya namna gani uliyo nayo? Je, nyumbani, kazini, sokoni na kanisani unadhihirisha roho ile ile, yaani, Roho ya Yesu Kristo, Mwanakondoo wa Mungu? Kama vile Yakobo na Yohana walivyoongozwa na Bwana Yesu, na sisi ‘tupokee kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zetu.’ (Yakobo 1:21).
Post a Comment