Mwalimu Christopher & Diana Mwakasege |
"Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena Bwana" (Warumi 12:19)
Kuna hasara zinazoweza kukupata ukiamua kulipa kisasi kwa mambo uliyofanyiwa ambayo hayakupendezi. Ikiwa ni masuala ya kikabila, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kidini, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kifamilia, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kikazi, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya uhusiano wako na majirani zako, usilipe kisasi.Ndiyo! Usilipe kisasi! Kwa nini? Kwa sababu "imeandikwa kisasi ni juu yangu Mimi; Mimi nitalipa, anena Bwana".
Lakini ikiwa utaona ya kuwa Mungu hawezi kukusaidia na ukaamua kujichukulia madaraka ya kujilipiza kisasi hasara zifuatazo hakika zitakupata!
Hasara ya Kwanza:
UTASHINDWA!
Katika jambo lolote lile lililokukasirisha - liwe la kidini, au kikabila, au kifamilia, au kikazi, na kadhalika ukiamua kulipa kisasi utashindwa wewe kwa sababu vita hivyo si vya mwili na wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili! Tunasema hivi kwa sababu katika 2 Wakorintho 10:3- 5 imeandikwa hivi:"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi yamwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo".
Tena katika kitabu cha Waefeso 6:12 imeandikwa hivi: "Kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho".
Uwanja wa mapambano uliyonayo ni "katika ulimwengu wa roho" na mapambano uliyo nayo "si juu ya damu na nyama" - ingawa unaona ya kuwa ni watu na ni binadamu kama wewe wanaokusonga - lakini fahamu hili ya kuwa wanatumiwa tu na ibilisi!
Mbinu mojawapo ya shetani anayotumia akitaka kukuangamiza ni kukufanyia kitu kitakachokukasirisha ili uamue kujibu au kushindana kimwili kwa sababu anajua ukishindana "kimwili" au katika mwili utashindwa hakika, maana vita hivyo si vya mwili wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili!
Hasara ya Pili:
MATATIZO HAYATAKWISHA!
Kumbuka imeandikwa hivi katika kitabu cha Wagalatia 6:7; "Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote ampandacho mtu. Ndicho atakachovuna".
Ikiwa umeamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule aliyekufanyia - ubaya hautakwisha, kwa sababu utavuna ulichopanda.Ndiyo maana imeandikwa hivi:"Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, mabaya
hayataondoka nyumbani mwake" (Mithali 17:13)
Ukiamua kulipiza kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nyumbani mwako - Biblia inasema "mabaya hayataondoka nyumbani mwako" Hii ndiyo maana matatizo mengi katika ndoa na katika jamii hayaishi - kwa sababu mtu akifanyiwa ubaya naye analipa kisasi.
Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nchini mwako ujue hakika mabaya hayataondoka nchini mwako. Hili ndilo lililowapata wenzetu wa nchi za Burundi na Rwanda - kulipizana kisasi - matokeo ni uhasama usiotaka kupotea - pamoja na juhudi zote za kimataifa kutafuta suluhisho.
Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa kazini kwako - fahamu mabaya hayataondoka kazini kwako. Ikiwa ni shuleni - mabaya hayataondoka hapo shuleni.
Tena hali ya mwisho inakuwa mbaya zaidi,kila wakati kisasi kinapoendelea kupandwa. Kwa sababu ukiwapa watu ubaya - nawe utapewa ubaya kwa; "kipimo cha kujaa na kushidiliwa, na kusukwa - sukwa - hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile upimacho ndicho mtakachopimiwa (Luka 6:38)
Kumbuka ubaya haushindwi na ubaya mwingine, bali unashindwa na wema - kama vile dawa ya chuki si chuki bali upendo! Ndiyo maana Warumi 12:21 inasema; "Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema".
Hasara ya Tatu:
UNAMZUIA MUNGU KUKUPIGANIA
Unaweza ukashangaa, lakini ndivyo ilivyo! Ukiamua kulipa kisasi juu ya tatizo ulilonalo - unamzuia Mungu asikusaidie kulitatua.Mungu hawezi kukusaidia kwa sababu imeandikwa "msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana, imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana".
Neno "ipisheni" limeandikwa kwa sababu kulipa kisasi "kunazuia" ghadhabu ya Mungu isipigane upande wako! Tena si hivyo tu lakini ukilipa kisasi unaingilia kazi ambayo si yako! Ni kazi ya Mungu maana anasema "Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana" Ikiwa kisasi ni juu ya Mungu kulipa, basi huhitaji wewe kulipa. Je, tunakwenda pamoja katika hili?
Hatua yako ya kulipa kisasi inazuia mkono wa Mungu kukupigania - kwa hiyo ipishe ghadhabu ya Mungu kwa kutokujilipizia kisasi!
Hasara na Nne:
UNAJICHUMIA DHAMBI!
Unapoamua kulipa kisasi, unajichumia dhambi! Hii ni kwa sababu kulipa kisasi huja kwa njia ya chuki iliyojengeka ndani yako kwa ajili ya mambo mabaya uliyofanyiwa. Huwezi kulipa kisasi bila ya kumchukia huyo unayejilipizia kisasi kwake. Na Biblia inasema hivi:
"Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajuaya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake" (1 Yohana 3:15).
Umeona hilo! Chuki huzaa kisasi, na huzaa dhambi ya kuua! Na
Isaya 59:2b inasema; "dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia".
Kwa hiyo kama umekwisha lipa kisasi au umekusudia moyoni mwako kulipa kisasi ni muhimu utubu ili Mungu akusamehe na mawasiliano yako na Yeye yawe mazuri.
HATUA TANO MUHIMU KATIKA KUSAMEHE
Biblia inatuambia kwamba Mungu huyu ambaye amesema anafuta na kuyasahau makosa yetu, kwa ajili yake mwenyewe, anakaa ndani ya watu wote waliompokea. Hebu soma na kutafakari maneno yafuatayo:
"Hapa mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno akafanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. ...... Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake, waliozaliwa,si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu" (Yohana 1:1, 14, 12, 13).
Yesu Kristo anapoingia ndani ya moyo wako, baada ya wewe kumwamini na kumpokea, unapewa uzima wa milele ndani yako, na unaanza maisha mapya.Imeandikwa kwamba, " Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya (2Wakorintho 5:17)
Utu mpya unazaliwa ndani yako, maisha, mawazo, matendo, maneno, yanatakiwa kubadilika Yesu Kristo aingiapo ndani yako. Pia, kusamehe kwako kunabadilika kunakuwa kupya.Lakini utaona kwamba watu wengi waliozaliwa mara ya pili, na kumkiri Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wao, bado wanaendelea kusamehe kama zamani.
Biblia inasema " ya kale yamepita, tazama!yamekuwa mapya"(2Wakorintho 5:17).
Kwa maneno mengine ni kwamba kusamehe kwako ulivyokuwa unafanya zamani, hakuhitajiki tena, tazama! Kusamehe sasa ni kupya. Tabia ni mpya.Zamani ulisamehe lakini bado ulikumbuka makosa uliyofanyiwa. Tena ulisamehe si kwa ajili yako bali kwa ajili yake aliyekukosea na wakati mwingine ulitaka uthibitisho kwanza kuwa kosa hilo halitarudiwa na ndipo usamehe. Ni lugha ya kawaida kusikia mtu akisema 'nasamehe lakini sitasahau'.
Katika maisha mapya utatakiwa usamehe na kusahau kwa ajili yako mwenyewe, ili kuomba kwako kusizuiliwe na baraka zako zisizuiliwe. Kwa kuwa imeandikwa hivi:
"Yeye asemaye yakuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda" (1Yohana 2:6)
Wewe unayesema kwamba una Kristo ndani yako, basi inakupasa kuenenda kama Kristo alivyoenenda alipokuwa hapa duniani katika mwili.Kwa kuwa Kristo alisamehe na kusahau, basi na wewe inakubidi kusamehe na kusahau.
Hatua tano zifuatazo zitakupa msingi imara wa kuishi siku zote katika upendo na amani na jirani zako na ndugu zako. Na pia, zitafungua milango mipya ya uhusiano wako na Mungu utakaoinua huduma yako katika kumtumikia Mungu. Na zaidi ya yote zitakuweka huru na magonjwa mengi yanayokusumbua:
1. Fahamu kuwa si wewe bali Kristo.
"Nimesulibiwa pamoja na Kristo, lakini ni hai, wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu" (Wagalatia 2:20)
"basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu" (Wakolosai 3:1-3)
Mistari hii michache ni baadhi tu ya ile inayotufunulia mambo yaliyofanyika ndani yetu tulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wetu.Si wewe unayeishi, bali ni Kristo aliye ndani yako. Na uhai ulio nao sasa, baada ya kuzaliwa mara ya pili, unao katika imani ya Mwana wa Mungu.Soma tena mstari huu:-
"..... Kwa maana mlikufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu."
"Kwa maana mlikufa." Utu wako wa kale, na mtu wa kale ndani yako alikufa siku ulipompokea Kristo maishani mwako. Kilichofuata ni uzima wa Kristo, katika utu mpya ukidhihirishwa katika maisha yako.Sasa unaweza kuelewa kwa nini Yesu Kristo alisema awachukiae ninyi, amenichukia mimi. ( Yohana 15 :18)
Mtu akikufanyia ubaya, usione kuwa anakufanyia wewe, ona kama vile Mungu aonavyo kuwa, ubaya huo anafanyiwa Kristo aliye ndani yako.Mtu akikutukana, akikusemea mabaya, akikupiga, fahamu kuwa si wewe anayekufanyia hayo, bali Kristo aliye ndani yako!Kuthibitisha haya Biblia inasema:
"Vita hivyo si vyako ni vya Bwana" (2 Mambo ya Nyakati 20:15). Ukiwa na wazo hilo katika roho yako, chukua hatua ya pili ifuatayo:
2. Mpende adui yako Umuombee
"Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako na umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi ...." (Mathayo 5:43, 44)
Jambo ambalo liko wazi ni kwamba hakuna msamaha wa kweli pasipo upendo,
"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtuma Mwanae ..." (Yohana 3:16)
Kilichomfanya Baba Mungu kumtuma Yesu Kristo duniani ni Upendo. Alitupenda sisi mno, alitupenda upeo wakati bado tulipokuwa tungali wenye dhambi. Na kuudhihirisha upendo huo, Yesu Kristo alizaliwa duniani na kufa masalabani ili sisi tupone.
Msamaha wa kweli unadhihirisha upendo ulio ndani ya mtu. Pasipokuwa na upendo, kusameheana hakupo. Palipo na upendo wa kinafiki, pia pana kusameheana kinafiki.
Kusameheana hakuonekani siku hizi, katika ndoa, kati ya ndugu, kati ya majirani, kati ya watu wa Mungu, KWA SABABU UPENDO WA WENGI UMEKWISHA POA!
Watu siku hizi wanafanya kile ambacho Yesu Kristo aliwaambia wasifanye. Yesu alisema, " Wapendeni adui zenu." Lakini, unaona katika watu wa Mungu, chuki imejaa, ndoa zinaharibika kwa sababu ya chuki, undugu unakufa kwa sababu ya chuki. Na ni hao wanaosema kuwa wameokoka na Yesu Kristo yumo ndani yao. Usiwachukie wanaokuudhi, wapende.
Yesu Kristo anakuambia watu wa dunia wanawapenda wanaowapenda na kuwachukia wanaowachukia, lakini wewe si wa dunia hii, wapende hata wale wanaokuchukia na ili kuonyesha kuwa unawapenda kweli, uwaombee!
Kwa nini Yesu Kristo, alisema "Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi?"
Ni,
"Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je? Nao hawafanyi kama hayo?" (Mathayo 5:45- 47).
Ulipompokea Kristo, ulipokea upendo mpya ndani yako, unaokuwezesha kufanya mambo ambayo mtu wa kale aliyekuwa ndani yako asingeweza kufanya. Mtu mpya ndani yako ana upendo mpya.
Upendo huu mpya, una tabia mpya, na mambo mapya.
"Upendo huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu; upendo hautakabari; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli huvumilia yote; huamini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote"(1Wakorintho 13:4 - 8).
Upendo huu umo ndani yako, na ndio unaokufanya uwe kiumbe kipya. Ni upendo ulio hai (Warumi 5:5)
Ni upendo unamuondolea mtu chuki, uchoyo na ubinafsi.
Kwa upendo huu, Bwana Yesu anataka uwapende adui zako, na kuwaombea pia ili wasamehewe na Mungu juu ya makosa waliyoyafanya.
Kwa upendo huu fanya yale ambayo ulikuwa huyafanyi zamani.
Kama ulikuwa husalimiani na adui yako, chukua hatua ya upendo, msalimie na ikibidi mtembelee nyumbani mwake. Kula pamoja naye, furahi pamoja naye, na omba pamoja naye.
Kuna watu wengine hawasalimiani wala kutembeleana na wazazi wao, au baba au mama, kwa sababu ya mambo yaliyofanyika zamani ambayo hawakuyapenda.
Sasa, chukua hatua waandikie barua, na uwatembelee kwa maana upendo wa Kristo umekuweka huru, na chuki na kinyongo.
Kumbuka unayafanya hayo kwa ajili yako mwenyewe ili maombi yako yakubaliwe mbele za Mungu.
Nafahamu kwa jinsi ya mwili, na kwa kutumia akili ya kibinadamu hatua hizo ni ngumu kuchukua.
Ni kweli, lakini kumbuka si wewe unayeishi, bali Kristo ndani yako. Na unayaweza yote (pamoja na kuwapenda adui zako) katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13)
Upendo unavunja nguvu za uadui. Usimuone jirani au ndugu ni adui tena. Kama vile wewe ulivyo kiumbe kipya ndani ya Kristo, kwa jicho la upya huo waone adui zako kuwa ni rafiki. Anza uhusiano mpya nao.
" Lakini nawaambia ninyi mnaosikia wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi" (Luka 6:27,28)
3. Samehe na Kusahau:
Wakati fulani nilikuwa mahali nikifanya semina ya neno la Mungu. Mtu mmoja akanifuata na akaniambia anataka nimuombee.
Nikamuuliza; "Nikuombee nini?"
Akasema; "Mimi shida yangu ni kwamba naona imani yangu ni ndogo na haikui, na maombi yangu hayajibiwi. Kwa hiyo naona nina shida katika maisha yangu ya kiroho, uniombee".
Inawezekana hata wewe una shida ya namna hiyo, kwa hiyo tafakari kwa makini maneno haya.
Niliahidi kumuombea baadaye kwa maana muda ulikuwa umekwisha.
Siku moja nilipokuwa ninaomba kwa Mungu juu ya shida yake, Bwana akanijibu katika roho yangu kuwa:
"Mtu huyo ana matatizo ya ndoa na kuna jambo lililomuudhi. Yeye anafikiri amesamehe, lakini bado ana uchungu moyoni mwake. Mwambie asamehe na kusahau na shida yake itakwisha".
Nilipowasiliana naye juu ya jambo hili, alikubali kuwa, ni kweli mwenzie amekuwa akimkosea mara kwa mara katika ndoa yao. Lakini alisema amekwisha msamehe.
Nikamuuliza; "Je! mbona basi kila mkikosana unakumbusha makosa ya nyuma?"
Akajibu; "Ni kweli, sasa nifanyeje wakati naona kila wakati makosa aliyonifanyia nyuma yakinijia kichwani?"
Hili ni tatizo la wengi. Na hujikuta wanasema wamesamehe kumbe bado. Msamaha si jambo la akili ni hatua ya rohoni. Ni uamuzi unaotoka ndani ya moyo wako.
"Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambiii hata mara saba, bali hata saba mara sabini" (Mathayo 18:21, 22)
"Na kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba , akisema, nimetubu msamehe. Mitume wakamwambia Bwana tuongezee imani" (Luka 17:4,5).
Mistari hii inatuonyesha jinsi kukua kwa imani, kunavyohusiana sana na kusamehe.
Wanafunzi walimwambia Bwana Yesu, awaongezee imani. Kwa kuwa walifahamu kwamba, kwa uwezo wao wasingeweza kusamehe kama Kristo anavyotaka.
Ni kweli kabisa.
Kama vile unavyohitaji imani katika kuomba, vile vile katika kusamehe na kusahau unahitaji imani.
Ulipompokea Kristo ulipokea kiasi cha imani (Warumi 12:3)
Na ili iongezeke unahitaji kusoma neno la Mungu na kulitenda. Imani huja kwa kusikia Neno la Mungu. (Warumi 10:17).
Imani ni ya rohoni na kusamehe ni kwa rohoni.
Unawezaje kusamehe na usiyakumbuke uliyofanyiwa?
Hilo ndilo tatizo kubwa alilokuwa nalo yule mtu aliyeniambia niomuombee. Na wengi pia wana tatizo la namna hii, na limekwamisha uponyaji na majibu mengine ya maombi yao, wameombewa mara nyingi, lakini bila mafanikio.
Kusamehe na kusahau ni kitendo cha imani ambacho ni budi kionekane kwa njia ya matendo ya mtu.
Kusamehe ni uamuzi wa mara moja na kusahau ni vita vya imani.
Sasa, utaniuliza, Ndugu Mwakasege, utawezaje namna hiyo?
Kabla sijakujibu, na mimi nakuuliza swali.
Siku ulipotubu dhambi zako, ulikuwa na uhakika gani ya kuwa Mungu amekusamehe wala hazikumbuki dhambi zako tena?
Utasema kwa kuwa ukitubu Mungu anasamehe.
Ni sawa kabisa. Hata mimi nakubaliana na hilo.
Lakini, je! Unaona kuwa Mungu anaweza kukuambia ufanye kitu ambacho anajua huwezi kukifanya?
Hapana hata kidogo. Bwana wetu si dhalimu!
Anafahamu kuwa WEWE MWENYEWE HUWEZI, LAKINI YEYE KWA KUWA YUMO NDANI YAKO ATAKUWEZESHA KUSAMEHE NA KUSAHAU.
Unayaweza yote katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13)
Ukiisha amua kumsamehe mtu hakikisha kwamba hulisemi tena jambo hilo katika kinywa chako.
Kumbuka kinywa kinanena yaujazayo moyo (Mathayo 12:34)
Na hayo maneno ndiyo yamtiayo mtu unajisi (Mathayo 15:18 - 20)
Usitafakari wakati wo wote ule, kosa ulilofanyiwa; mawazo mabaya yanapokujia juu ya kosa ulilofanyiwa, fahamu kuwa ni shetani na nafsi yako tu.
Biblia inasema mpingeni shetani naye atawakimbia (Yakobo 4:7)
Na wala msimpe nafasi (Waefeso 4:27)
Mwambie shetani aondoke na mawazo yake, kwa kuwa hilo kosa umelisamehe na kulisahau.
Na wakati huo utafakari nini?
"Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote ya kupendeza, yo yote yenye sifa njema, ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, YATAFAKARINI YAYO" (Wafilipi 4:8)
"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili; bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha MAWAZO na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na TUKITEKA NYARA KILA FIKRA ipate kumtii Kristo" (2 Wakorintho 10:3 - 5)
Kusahau ni vita vikali vya imani vinavyopiganwa katika mawazo yako. Unaposhinda vita hivi, unajikuta umepiga hatua kubwa ya imani!
KWA HIYO KUMBUKA:Unasamehe kwa ajili yako Mwenyewe.
Na unasahau makosa uliyokosewa kwa ajili yako mwenyewe.
Kumbuka hili kila wakati, unamsamehe aliyekukosea na kuyasahau aliyokukosea kwa ajili yako mwenyewe.
Na kila wakati wazo likija kukukumbusha kosa hilo likatae kwa Jina la Yesu. Na USIKUBALI KULISEMA TENA MAISHANI MWAKO.
4. Hasira ipeleke kwenye maombi
"Mwe na hasira, ila msitende dhambi jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi" (Waefeso 4:26, 27)
Mwe na hasira, ila msitende dhambi, ni mstari ambao watu wengi wameutumia vibaya. Kutokana na maneno hayo wamefanya vitendo vingi viovu kwa mawazo, maneno na kwa matendo.
Biblia haiwezi kujipinga yenyewe. Roho Mtakatifu ndiye aliyewaongoza watu kuandika maandiko hayo Matakatifu.
Lakini, soma mistari ifuatayo:
"Uchungu wote na ghadhabu na HASIRA na kelele na matukano YAONDOKE KWENU" (Waefeso 4:31)
"..... HASIRA ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu" (Yakobo 1:20)
"Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya HASIRA watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu" (Wagalatia 5:19 -21)
Hapa unaona jinsi hasira ilivyofananishwa na uchawi, uasherati, uadui, ibada ya sanamu, na mambo mengine kama hayo ambayo yanamzuia mtu asiurithi ufalme wa Mungu.
Na Yesu Kristo akikaza ubaya wa hasira alisema:
"Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, kila amwoneaye ndugu yake HASIRA itampasa HUKUMU" (Mathayo 5:21, 22)
Yesu anasema ukiwa na hasira unastahili hukumu, lakini Roho aliyesema ndani ya Kristo, ni huyo huyo aliyesema ndani ya Paulo kuwa, "Mwe na hasira, ila msitende dhambi".
Je! Unafikiri biblia inagongana yenyewe? Hapana! Paulo alikuwa ana maana gani aliposema tuwe na hasira lakini tusitende dhambi? Unawezaje mtu ukawa na hasira lakini usitende dhambi?
Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya magonjwa na hasira.
Ngoja nikueleze jinsi mimi yalivyonitokea.
Mara tu mimi nilipompokea Kristo katika roho yangu, kulikuwa na kitu kimoja kilichokuwa kikinisumbua. Ilikuwa mtu akiniudhi nilikuwa nakasirika haraka sana. Na wakati wote nitakuwa nalifikiria jambo hilo moyoni mwangu.
Mwisho wake nilikuwa naona uchungu unaingia moyoni mwangu.
Sasa kila mara nilipokasirika nilikuwa nashindwa kuomba na mara ninaanza kuumwa homa.
Jambo hili lilinisumbua muda mrefu. Kila nikitubu na kumsamehe aliyenikosea, na kuliacha hilo mikononi mwa Mungu; ugonjwa niliokuwa nao ulikuwa unapona.
Nilifahamu kitu kimoja kuwa nikiweza kulitatua tatizo la hasira, ugonjwa huo hautaniruida tena. Kwa kuwa ulikuwa unakuja mara tu nikikasirika.
Nikawa na tatizo la hasira mikononi mwangu.
Kwa hiyo, nikamlilia Mungu katika maombi juu ya shida hii.
Watu wengi wanatatizo la namna hii, kila wanapokasirika juu ya jambo fulani, wanaugua. Utakuta wengi wakikasirika wanaumwa vichwa, vidonda vya tumbo, kifua, moyo, damu kwenda mbio, homa, na magonjwa mengine.
Tatizo si ugonjwa hapo.Tatizo ni hasira!
Nilipokuwa nikiomba, Roho wa Bwana alinipa jibu na naamini kuwa kama nilivyosaidiwa mimi na wewe utapata msaada. Na ndiyo maana nimekushirikisha hili.
Unapoona kuwa kuna jambo limekuudhi, usiwe mwepesi kujibu au kufanya kitu. Tulia kimya na tafuta nafasi uanze kuomba.
Kwanza tubu kwa Baba juu ya kukasirika kwako, na pili, mwambie Baba jinsi unavyojisikia moyoni mwako, bila kumficha kitu, na tatu, mwombe kitu ambacho unataka akufanyie katika jambo hilo.
Utajikuta unapoomba na kuumimina moyo wako kwa Bwana, Yeye ataichukua hiyo hasira uliyokuwa nayo na uchungu wote. Na badala yake anahuisha upya upendo mpya ndani ya moyo wako utakaokuwezesha kupita juu ya tatizo ulilo nalo.
Ukiona bado hasira inatokea, ikemee kwa jina la Yesu, na itatoweka.
Paulo aliposema, Mwe na hasira, ila msitende dhambi hakuhalalisha ya kuwa hasira ni nzuri.
Kwa maneno mengine alikuwa akisema kuwa unapopata uchungu kwa kuudhiwa angalia usifanye vitendo vitakavyomuaibisha Kristo.
Kwa kuwa kuudhiwa kupo maadamu upo duniani, na kwa mtu wa Mungu maudhi yanazidi. Lakini Paulo anasema watu wajue namna ya kuishughulikia hasira inapokuja kutokana na maudhi.
Ndiyo maana aliendelea kusema:
"Jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka, wala msimpe ibilisi nafasi" (Waefeso 4:26,28)
Usimpe ibilisi nafasi kwa kuiacha hasira ikazaa ugomvi, matusi na fitina.
Uchungu huo utautoaje?
Usiupeleke kwa aliyekuudhi, wala usikae nao. Upeleke kwenye maombi na upendo utavuma baada ya Mungu kuondoa uchungu uliokuwa nao.
Kuna wengine wanasema hasira aliyonayo ni ya ukoo kwa kuwa ndugu zake waliomtangulia wana hasira.
Kuna wengine huwa wakikasirika kuna kitu kinapanda na kikifika shingoni kinamfunga asiseme, na anaanza kupumua kwa nguvu na wakati mwingine huanza kulia.
Ukiona namna hiyo, chukua silaha mkononi ya Jina la Yesu na ukemee. Maana hiyo ni roho ya shetani iliyojifunika katika hasira.
Hakuna hasira ya ukoo kwa watu wa Mungu, ambao ni uzao mpya katika uzao wa Mungu. Ukoo wako ni ukoo wa Mungu. Ni ukoo wa Upendo si wahasira.
Baada ya mimi kuchukua hatua hizo, ule ugonjwa sijauona tena, na hasira sikuiona kunifuatafuata kwa kuwa niliacha kuwatizama watu kwa jinsi ya mwili, bali nilianza kuwatambua kwa jinsi ya rohoni (2Wakorintho 5:16)
5. Furahi siku zote.
Siri ya ushindi katika matatizo yoyote, inatokana na furaha ya Kristo iliyo ndani ya mtu.
Neno la Mungu linasema, "Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema, Furahini" (Wafilipi 4:4)
" Heri ninyi watakpowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia;kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu" (Mathayo 4:11, 12)
Huu ni ujumbe mzuri sana wa Bwana Yesu, kwa mtu wake aliyesongwa na maudhi pamoja na makwazo mbali mbali.
Inawezekana kuwa ndani ya nyumba yako una makwazo ya kila siku, kutokana na mume wako au mke wako ambaye hatembei katika nuru ya Kristo.
Na pia, inawezekana unapata maudhi sana juu ya tabia za watoto wako, ambao hawaenendi katika kweli ya neno la Mungu. Inawezekana unapata maudhi shuleni au kazini.
Hata kama umesongwa na makwazo na maudhi namna hiyo, Yesu Kristo , aliye bwana na Mwokozi wako, anakuambia. "FURAHI NA KUSHANGILIA".
Furahi na kushangilia katika Bwana siku zote na katika yote. Hii ndiyo siri ya ushindi.
Kwa nini ufurahi na kushangilia?:
Kwa kuwa unafahamu kuwa mgomvi wako si mtu bali ni shetani. (Waefeso 2:1 - 3).
Kwa kuwa unafahamu kuwa anayekuudhi si mume wako, wala mke wako, wala watoto wako, bali ni shetani anayewatumia kutaka kukukasirisha wewe, ili umkosee Mungu wako.
Kwa kuwa unafahamu kuwa shetani ameshindwa; na wewe una mamlaka juu yake na maudhi yake yote (Luka 10:19)
Kwa hiyo ufanyeje?
Furahi na kushangilia moyoni mwako.
Kumbuka kuwa Kristo aliye ndani yako ni mkuu kuliko shetani na makwazo yake na maudhi yake (1Yohana 4:4).
Furahi na kushangilia unapoudhiwa, na mtolee Mungu shukrani kwa nyimbo za sifa.
Fanya hivyo na hasira haitapata nafasi moyoni mwako, wala uchungu wo wote.
Tumia tabia ya Kristo iliyo ndani yako ya kuwaombea wanaokuudhi, kama vile yeye alivyosema pale msalabani, "Baba uwasemehe kwa maana hawajui walitendalo".
Baada ya kufurahi na kushangilia na kusifu, kitu gani kinafuata?
"Upole wako ujulikane na watu wote" (Wafilipi 4:5)
Na upole ni tunda la Roho. Na kazi ya roho ya upole ni kutuliza maudhi. (Mhubiri 10:4)
Wakati wa maudhi ndiyo wakati mzuri wa kumdhihirisha Kristo aliye ndani yako katika upole wote na utulivu.
Usijisumbue na kuhangaika katika neno lo lote, bali katika kila jambo, kwa kusali na kuomba na kushukuru, haja yako na ijulikane na Mungu (Wafilipi 4:6).
Usiwe mwepesi kumwambia mtu maudhi ya nyumbani mwako, au ofisini mwako. Utajikuta umeingia katika kusengenya na hutafaulu kamwe kujifunza kusamehe.
Maudhi na makwazo yapeleke kwa Bwana. Yeye anatosha kukushindia.
Fanya hivyo, na amani ipitayo akili na fahamu zote na maudhi na makwazo itakuhifadhi na kukufariji moyo wako siku zote katika Bwana (Wafilipi 4:7)
Nilikuwa mahali fulani nikifundisha neno la Mungu, na kila siku niliombea wagonjwa. Basi, siku moja mama mmoja alisimama kushuhudia alivyopona.
Na haya ndiyo aliyosema:
"Nina uhakika kuwa ugonjwa huu niliokuwa nao ulikuja kwa sababu ya dhambi nilizokuwa nazo. Mimi sikushikwa na dhambi zingine kama wengine wanavyoshikwa. Mimi nilishikwa na dhambi hii.
Mume wangu huwa hanipi fedha ya kununulia chumvi nyumbani. Basi nilichukia sana; na mimi nikipata fedha na kununua chumvi, naificha nje ya nyumba. Mimi na watoto tunakula chakula chenye chumvi. Mume wangu namtengea chakula kisichokuwa na chumvi.
Na niliwambia watoto ye yote atakayesema hayo kwa baba yake atachapwa.Lakini nilipoanza kufanya hivyo nilianza kuugua mara kwa mara, na hapa kwenye mkutano huu nimekuja na mguu umevimba na kunisababisha nisitembee vizuri.
Baada ya kusikia neno la Mungu nilifahamu kuwa ugonjwa huu nimeupata kwa sababu ya kosa hilo la kumkasirikia mume wangu.
Nikamsamehe mume wangu. Nikatubu kwa Mungu. Na maombezi ya wagonjwa yalipofanywa nilijikuta nimeanguka chini. Nilipoamka nilikuta uvimbe mguuni umetoweka. Na sasa nimepona na natembea vizuri.
Nikirudi nyumbani nitamwambia mume wangu yote, na nitamwomba anisamehe".
Hii ndiyo nguvu ya uponyaji ya neno la Mungu inayoshuka baada ya kusamehe. Roho zinapona, miili inapona na ndoa zinapona! Yule mama alisamehe kwanza ndipo akapokea uponyaji.
Na wewe sasa, samehe na kusahau upokee uponyaji wako au upokee majibu ya maombi yako.
Kumbuka kabla ya kusimama na kusali samehe kwanza. Hii ni kwa ajili yako mwenyewe, ili usamehewe na Mungu na upokee unaloomba siku zote
Post a Comment