KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU
Watu wengi hasa waliookoka wamekuwa wakishindwa kuelewa nini hasa maana ya karama na kwa sababu hiyo wamejikuta wakitafsiri vibaya maana yake na kusababisha migogoro ndani ya makanisa yao. Hawakusudii kuwa na migogoro bali ni kwa sababu ya kutojua hasa maana ya neno ‘karama’. Kabla ya kuendelea na karama za Roho Mtakatifu ni muhimu tujifunze maana ya neno ‘karama’.
Katika kamusi ya Kiswahili Sanifu neno ‘Karama’ limetafsiriwa kama “Kipawa anachokuwa nacho mtu kwa sababu ya kumwabudu sana Mungu agh. Humpa uwezo wa kuomba haja kwa Mwenyezi Mungu na kukubaliwa mara moja; ikibali ya kupokewa haja iombwayo” na neno ‘kipawa’ linatafsiriwa kama “uwezo mtu aliozaliwa nao ambao humwezesha kufanya jambo Fulani vizuri”.
Katika kamusi ya kiswahili kwa kiingereza, neno ‘karama’ limetafsiriwa kama gracious gifts likiwa na maana ya zawadi za neema, ‘Neema’ ni kustahilishwa bila kustahili au bure. Kwa hiyo zawadi za neema ni zawadi ambazo mtu anazipata bila kustahili au kuzigharimia. Maana yake mtu anapata zawadi kwa sababu aliyempa ameamua kumpa na kwamba anaweza kunyimwa yeye na akapewa mwingine na hawezi kudai kwa sababu siyo haki yake.
Kwa jinsi hiyo basi karama za Roho Mtakatifu ni zawadi ambazo Roho Mtakatifu huwapa watu (wakristo wamwabuduo sana) kwa neema na ndiye huamua ampe nani, zawadi gani bila kujali anapenda au hapendi. Tatizo la waskristo kung’ang’aniana karama na kugombana siyo mpango wa Mungu kwa sababu karama hutolewa na Roho Mtakatifu kadri apendavyo yeye.
Kutokana na maelezo haya ni dhahili kwamba watu tofauti hupewa karama tofautitofauti kwa kadri Roho Mtakatifu apendavyo na hakuna sababu ya kung’ang’ania karama au kulazimisha kutaka kuwa na karama fulani. Mkristo akiwa mwaminifu mbele za Mungu, Roho Mtakatifu atampa karama kama apendavyo yeye mwenyewe (Roho). Paulo Mtume aliwaambia Wakoritho,
''…maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa apendavyo Roho yeye yule''. (1Wakorintho 12:8).
Petro naye anasema,
“kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana....'' (1 Petro 4:10).
Watu wanaweza kujiuliza kuwa karama za roho Mtakaitfu ni za kazi gani au kwa nini tuwe nazo katika kanisa? n.k., sababu zipo, Mungu hafanyi kitu chochote bila sababu ya msingi.
Roho Mtakatifu huzileta karama hizo katika kanisa kwa ajili ya kurahisisha ujenzi wa kanisa lake pamoja na kazi zake. Ili kanisa lijengeke, tunahitaji karama mbalimbali za Roho Mtakatifu. Karama zipo tofautitofauti na zinafanya kazi kwa kushirikiana kulijenga kanisa.
“Vivyo hivyo na ninyi kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni sana kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa”. (1 Wakoritho 14: 12).
Kanisa linapokosa karama za roho mtakatifu ni lazima lisijengeke na kazi ya Mungu isiendelee mahali hapo; kanisa linadumaa na watu wanakwenda kama vipofu wasiojua kwa kwenda na viziwi wasiosikia chochote.
Wakristo tunapaswa kuzifahamu karama za Roho Mtakatifu ili tuone zikifanya kazi ya kulijenga kanisa na tunapaswa kutamani kuwa nazo ili kulijenga kanisa (1Wakoritho 14:12). Karama zisipofahamika, ni viigumu kulijenga kanisa.
“Basi ndugu zangu kwa habari ya karama za Roho sitaki mkose kuzifahamu” (1Wakorotho 12:1).
Katika utendaji kazi wa Roho Mtakatifu, mambo yafuatayo ni ya muhimu sana kuyafahamu vizuri,
I. Fahamu na kubali kwamba karama za Roho zinaweza kufanya kazi hata kwako: Roho Mtakatifu anazo karama zote na humgawia kila mtu kama apendavyo yeye mwenyewe.
“Basi pana tofauti kati ya karama, bali Roho ni yeye Yule …lakini kazi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye”(1Wakoritho 1:4, 11).
Kwa kuwa Roho ndiye agawaye, basi hapana sababu ya kutaka zaidi ya agawavyo Roho.
“kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita iliyompasa kunia …, basi kuwa tuna karama zilizo mbalimbali… (Warumi 12:3-6).
II. Uwe na hamu kubwa ya kusaidiwa na Mungu: Ili karama za Roho Mtakatifu ziweze kufanya kazi yake, ni lazima mwamini awe na hamu ya kutaka msaada wa Mungu. Lazima ajue kwamba yeye hawezi peke yake isipokuwa Mungu amemsaidia na hivyo aombe msaada wa Mungu. Kumbuka huwezi kuwa na karama za Roho zikafanya kazi kama hukuomba msaada wa Mungu akusaidie.
''Ufuateni upendo na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu, vivyo hivyo na ninyi kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa''.(1 Wakorintho 14:1, 12)
III. Kwa kadri ya imani yako karama zitatenda kazi vizuri (imani yako itasaidia): Karama hutenda kazi ndani ya mtu kutegemeana na kiwango cha imani alichonacho. Unapokuwa na imani kubwa na thabiti, karama za Roho Mtakatifu zinatenda kazi zaidi.
“Basi kwa kuwa tuna imani zilizo mbalimbali … ikiwa unabii tutoe unabii kwa kadri ya imani. (Warumi 12:6).
Unaposikia Neno la Kristo ndipo unapopata imani ya kukusaidia kutembea katika karama.
“Imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa Neno la Kristo”. (Warumi 10:17).
Haitakiwi kutembea kwenye karama zaidi ya imani aliyonayo mtu hutoka katika Neno la Kristo. Ukifahamu Neno la Kristo kwa wingi utaamini na kutembea katika karama kwa kadri ya imani hiyo.
“…Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo.” (1 Wakoritho 12:8).
“Kila mmoja na atumie kipawa cho chote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.” (1 Petro 4:10).
IV. Jifunze jinsi roho anavyowasiliana nawe: mawasiliano baina ya Roho Mtakatifu na mkristo (aliyeokoka) hayako mbali kwa sababu mbalimbali, kwanza mkristo ni hekalu la Mungu; pili, Roho Mtakatifu anakaa ndani ya mkristo;
'' Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?'' (1Wakorintho 3:16).
Hapa kuna vitu vinne ambavyo ni mtu, nafsi, roho na mwili. Mtu ni Roho na kwake kuna nafsi na anaishi katika mwili. Roho Mtakatifu pia yupo katika mwili. Nafsi ndiyo inayotawala mwili na kazi yake ni kufafanua/kutafsiri ambacho mwili unataka kwa lengo la kuieliewesha roho na pia kuelewesha mwili kile ambacho roho inataka mwili uelewe. Kazi ya nafsi ni kubwa kwa kuwa ndiyo inayounganisha mwili na roho (mtu). Hii inamaanisha kuwa vyovyote utakavyotenda ni matokeo ya tafsiri ya nafsi. Hivyo basi nafsi inahitaji msaada. Nafsi inasaidiwa kwa kulisoma Neno la Mungu. Fikra za nafsini ndizo zinazoathiri mwili na roho.
''Naye Yesu, alipoiona imani yao, ........ wakifikiri mioyoni mwao ..... Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao .....''.(Marko 2:5-8).
Paulo naye aliwaambia Wagalatia;
''Tangu sasa mtu asinitaabishe kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu” (Galatia 6:17).
V. Ujazo wa nguvu za Roho Mtakatifu lazima uwe endelevu:Ujazo wa nguvu za Roho Mtakatifu wa siku moja hauwezi kutosheleza. Inapaswa kila wakati kuwepo nguvu mpya.
''Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung'unika, kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama,........... mtu akihudumu na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu, .......'' (I Petro 4:9-11).
Tunapaswa kuhudumu kwa nguvu tunazojaaliwa kila siku na hivyo ni lazima tuende mbele za Mungu kila wakati ili kujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu. Kuna kiwango cha nguvu ya Roho mtakatifu ndani ya mtu hakiwezi kusukuma karama fulani za Roho Mtakatifuili ziweze kufanya kazi au kuhudumu; tunahitaji kujazwa kila wakati.
Karama za Roho Mtakatifu zinaweza kufafanuliwa kwa namna mbalimbali. Hapa tunafafanua karama za Roho Mtakatifu kama vipawa au zawadi ambazo Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu anawapa wakristo kwa ajili ya kulijenga kanisa lake. Karama ni vipawa kwa sababu uwezo huo anaoupata mtu si wa kawaida na si wote wanaweza kuwa nao isipokuwa wale tu waliopewa; ni zawadi kwa sababu mtu yeyote (mkristo/mwamini) anaweza kupewa kama Roho Mtakatifu apendavyo na si haki ya kudai upendavyo.
Kazi kubwa ya karama ni kwa ajili ya kulijenga kanisa lililo kusudi la kuja kwa Roho Mtakatifu.
''Vivyo hivyo na ninyi kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa''. (1Wakorintho 14:12).
Karama za Roho Mtakatifu hazifanyi kazi kwa ajili ya mtu binafsi bali kwa ajili ya kulijenga kanisa na si kwa mapenzi ya mtu binafsi bali kwa mapenzi ya Roho.
“Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye''. (1 Wakoritho 12:11).
Karama za Roho Mtakatifu zimeorodheshwa katika barua ya kwanza ya mtume Paulo kwa Wakoritho kama inavyosomeka:
“Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani kwa Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Ruho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza, na mwingine unabii, na mwingine kupambanua Roho; mwingine aina za lugha, na mwingine tafsiri za lugha”. (1Kor 12:7-10).
Orodha nyingine zipo katika: 1Wakoritho 12:26-30; Waefeso 4:11.
“Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake. Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatuwaalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?”(1Wakoritho 12:26-30)
Hapa tunapata karama zenye sehemu ya kipekee kabisa katika huduma ya kulijenga kanisa. Ili kuzielewa karama hizi zitafafanuliwa moja baada ya nyingine;
Kazi ya karama ya Neno la maarifa ni kutoa habari ya mambo yaliyopo na yaliyopita ili kusaidia kutambua hila zilizojificha zikitaka kukwamisha utumishi na kupotosha maamuzi. Karama ya maarifa husaidia kufanya maamuzi yaliyo sahihi. Pia husaidia kujua maswali waliyonayo watu na mahitaji yao bila kuambiwa nao.
Karama ya Neno la maarifa hufanya kazi kwa njia nne ambazo ni;
i) Kwa njia ya mawazo,
ii) Kwa njia ya ndoto,
iii) Kwa njia ya maono, na
iv) Kwa njia ya kuuweka mwili wako katika hali aliyonayo mwenye uhitaji.
Kumbuka kuwa karama hufanya kazi kwa kushirikiana. Hebu tuone jinsi ambavyo karama ya neno la maarifa inavyofanya kazi.
Hii ni njia ambayo hutumika mara nyingi zaidi; angalia,
''.......mara (ghafla) Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao.....'' (Marko 2:6-8).
Maana yake ni kwamba alipata wazo jingine tofauti na alilokuwa akiliwaza wakati ule, yaani Roho Mtakatifu alilileta wazo hilo jipya ndani yake.
Yahana alipokuwa akihubiri kando ya mto Yordan, watu walianza kujiuliza mioyoni mwao ikiwa Yohana angeweza kuwa ndiye Kristo, lakini Yohana bila kuambiwa na mtu aliweza kuyajibu maswali yao kwa sababu Roho Mtakatifu aliyaleta ndani yake.
“…Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yohana angeweza kuwa ndiye Kristo. Yohana akawajibu akawaambia, ‘‘Mimi nawabatiza kwa maji Lakini atakuja aliye na nguvu kuliko mimi ambaye sistahili hata kufungua kamba ya viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.” (Luka 3:15-16).
Hapa Yohana hakuulizwa swali na mtu yeyote bali alijibu swali lililoletwa ndani yake na Roho Mtakatifu.
Walimu wa sheria na viongozi wa makuhani walitaka kumtega Yesu wapate kumkamata na kumshitaki, lakini Yesu alitambua na kuwashinda;
“…Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa waaminifu ili wapate kumtega kwa maneno asemayo ili wamtie katika uwezo na mamlaka ya mtawala. Hivyo wale wapelelezi wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu kwa kufuata ukweli. Je, ni halali sisi kumlipa Kaisari kodi au la?” Lakini Yesu akatambua hila yao… Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu Yake, wakanyamaza kimya.” (Luka 20: 18 - 26).
Mawazo yalimjia Yesu kuhusu nia yao au Yesu aliwaza kile walichokuwa wakikiwaza wao.
Neno la maarifa kwa njia ya mawazo inahitaji kujizoesha kukabidhi mwili wako, roho yako na nafsi yako kila siku mbele za Mungu na omba kuwa na usikivu (sensitivity), utulivu, na kufundishwa na Mungu kutembea katika karama hiyo.
Ndoto ni mtiririko wa taswira au matukio ambayo hujitokeza bila hiyari katika ubongo wa mtu akiwa usingizini; kwa kawaida ni mchanganyiko wa wahusika halisi na wale wa kufikirika (Encarta Dictionaries, 2008).
Tafsiri hii inajengwa na mambo makuu manne, nayo ni:
- Ndoto ni lazima yawe matukio au taswira,
- Ndoto hutokea bila hiyari katika ubongo wa mtu,
- Ndoto hutokea mtu akiwa usingizini, na
- Ndoto huhusisha wahusika halisi na wale wa kufikirika.
Roho Mtakatifu kwa kupitia ndoto huleta neno la maarifa, yaani kuwafahamisha watu mambo yaliyopita, yaliyopo, na au yajayo wakiwa katika usingizi. Bahati mbaya sana watu wengi (wakristo) hawajafahamu kuwa ndoto ni njia ambayo Mungu huzungumza nao kwa Roho Mtakatifu ili kulijenga kanisa yaani muumini mmoja mmoja hadi kundi kubwa. Kwa kutokujua watu wamedharau ndoto na kusababisha Roho Mtakatifu asiseme nao tena kwa kukosa utii na matokeo yake ni kanisa kukumbwa na matatizo na kushindwa kukua.
Tunawaona watumishi wengi wa Mungu katika Biblia jinsi ambavyo Mungu alisema nao kwa njia ya ndoto; hapa tutawaona baadhi yao tu.
Abimeleki kabla ya kumwingilia Sara mke wa Abraham, Mungu alimtokea katika ndoto akimwonya na kumjulisha kuwa yule ni mke wa mtu.
“Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto wakati wa usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua, yeye ni mke wa mtu.’’ Wakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, …. Kisha Mungu akamwambia katika ndoto, “Ndiyo, najua ya kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi…” (Mwanzo 20:3-6).
Yakobo akiwa anamkimbia ndugu yake Esau alifika mahali fulani, Mungu alisema naye kwa njia ya ndoto.
“…. Akachukua jiwe moja la mahali pale, akaliweka chini ya kichwa chake akajinyoosha akalala usingizi. Akaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake. Juu yake alisimama BWANA, akasema, “Mimi ni BWANA, Mungu wa baba yako Abrahamu na Mungu wa Isaki…..””. (Mwanzo 28:10-17).
Yakobo aliota ndoto ya kupatiwa mifugo mingi kama ujira wake kutoka kwa Labani.
“Wakati Fulani majira ya kuzaliana niliota ndoto ambayo niliinua macho Na kuona … Malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, ‘Yakobo’ nikamjibu, ‘Mimi hapa,’ akasema, ‘Inua macho yako uone wale mabeberu …”(Mwanzo 31:10-12).
Yusufu alikuwa akiota ndoto ambazo Mungu alikuwa akimwonyesha kuwa ndugu zake watakuja kumsujudia baadaye;
Yosefu akaota ndoto …. Akawaambia, ‘‘Sikilizeni ndoto niliyoota: Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafla mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ilizunguka na kuuinamia …. Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, ‘‘Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.’’ (Mwanzo 37:5-9).1
Sulemani anatokewa na Mungu katika ndoto akimtaka aombe chochote anachokitaka;
“BWANA akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, ‘‘Omba lo lote utakalo nikupe.’’ … Ndipo Solomoni akaamka, akatambua kuwa alikuwa katika ndoto” (Mwanzo 3:5-15).
Kuhusiana na kuzaliwa kwa Yesu Kristo, ndoto zilitumiwa na Mungu kuwajulisha watu wake habari za mambo mengi kama vile Yusufu kutomwacha mkewe, Mamajusi kutorudia njia ya Mfalme Herode baada ya kumwona Yesu, Yusufu kumtorosha mtoto Yesu asiuawe na Mfalme Herode, na Yusufu kurudi Israel baada ya Mfalme Herode kufa.
“… Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu”(Mathayo 1:20).
Nao (mamajusi) wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine. Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amwue.’’ Kisha Yosefu…”(Mathayo 2: 12-15).
“Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa”. (Mathayo 2:19-20).
Kabla ya Pilato kutoa hukumu yake juu ya Yesu, mke wake alikuja na kumwonya asifanye baya juu ya Yesu kwa sababu aliteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.
“Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: ‘‘Usiwe na jambo lo lote juu ya huyu Mtu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu Yake.”” (Mathayo 27:19).
Ndoto ni njia mojawapo ambayo pia Mungu hutumia katika kujibu maombi yetu mbele zake. Sauli anapokabiliwa na Jeshi la Wafilisti anamwomba Mungu shauri lakini biblia inasema Mungu hakumjibu kwa ndoto wala kwa urimu wala kwa njia ya manabii.
Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa, moyo wake ukajawa na hofu kuu. Lakini Sauli akauliza ushauri kwa BWANA, lakini BWANA hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa njia ya manabii. (1 Samw. 28:5-6).
Wakati mwingine ndoto huhitaji kutafsiriwa kwa sababu huja kama fumbo hasa inapotokea wahusika wake si binadamu kama vile mimea, wanyama, n.k. kwa mfano ndoto ya Farao kule Misri ilihitai kutafsiriwa ili kujua maana yake, vinginevyo Misri ingekumbwa na baa la njaa. Mfalme anashindwa kutafsiri lakini Yusufu anaifasiri;
Farao akamwambia Yosefu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia ikisemwa kwa habari yako kwamba unapoelezwa ndoto waweza kuifasiri.” Yosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.” …. Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto iyo hiyo moja…. Ng'ombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba, ni ndoto iyo hiyo moja.
Ng'ombe saba waliokonda na wabaya wale waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki, ni miaka saba ya njaa. (Mwanzo 41:15-16, 25-27).
Neno la maarifa kwa njia ya ndoto inahitaji kila wakati kuwa msafi mbele za Mungu ili aweze kusema nawe vinginevyo shetani anaweza kukuletea ndoto zake. Sauli hakujibiwa kwa sababu alijichafua. Kumbuka pia kuwa unahitaji kupima Roho yaani si kila ndoto inaletwa na Mungu na kipimo kizuri ni Neno la Mungu yaani Maandiko Matakatifu.
Neno maono jina linatokana na kitenzi ona lenye maana yatambua kwa macho. Maono yaweza kutafsiriwa kama mambo au vitu ambavyo vinatambuliwa kwa macho au kwa kifupi maono ni mambo yanayoonekana. Katika ulimwengu wa Roho maono ni vile vitu ambavyo Mungu kwa kupitia Roho Mtakatifu huwaonesha wakristo katika hali isiyo ya kawaida inayopita ufahamu wote wa kisayansi (supernatural apparition) kwa ajili ya kulijenga kanisa.
Maono hutokea tu pale ambapo mtu anakuwa mnyenyekevu mbele za Mungu; hutokea mtu akiwa macho isipokuwa tu kwamba akili yake inahamishwa kutoka katika mazingira yanayomzunguka akiona vitu na mambo ambayo hayapo hapo, wengine hawaoni. Kuna mifano mingi katika Biblia lakini tuangalie michache tu.
Yesu akiwa na wanafunzi watatu (Petro, Yakobo, na Yohana) alibadilka sura na ghafla wanafunzi wakawaona Musa na Elia (manabii waliokufa zamani) wakizungumza na Yesu;
“…. Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang'aa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho. Ghafula wakawatokea mbele yao Mose na Eliya, wakizungumza na Yesu. Ndipo Petro …. Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaagiza, ‘‘Msimwambie mtu ye yote maono haya mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuka kutoka kwa wafu.’’’ (Mathayo17:2-4, 9).
Yohana akiwa katika kisiwa kile cha Patmo alitokewa na Yesu katika maono na akaona mambo aliyoagizwa ayaandikie makanisa saba ya kule Asia. Katika maono yale Yohana anasema;
“Nilikuwa katika Roho siku ya Bwana, nikasikia sauti kubwa kama ya tarumbeta nyuma yangu ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha ukipeleke kwa makanisa saba, yaani: Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.’’ Ndipo nikageuka ili nioneni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu, katikati ya vile vinara vya taa, nikaona mtu kama Mwana wa Adamu, amevaa joho refu na mkanda wa dhahabu umefungwa kifuani mwake. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. …. Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akaweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema, “Usiogope, Mimi ni wa Kwanza na wa Mwisho” (Ufunuo 1: 10-17).
Baada ya Yohana kufunuliwa mambo aliyotakiwa kuyaandika kwa yale makanisa saba, Mungu aliendelea kumwonyesha maono mengine mengi sana akianza na kumwonyesha mlango ulio wazi wa Mbinguni. Akaonueshwa mambo ambayo hayana budi kutokea;
“Baada ya mambo hayo nilitazama, nami nikaona mbele yangu mlango uliowazi mbinguni. Nayo ile sauti niliyokuwa nimeisikia hapo kwanza ikisema nami kama tarumbeta ikasema, “Njoo panda huku nami nitakuonyesha yale ambayo hayana budi kutokea baada ya haya.’’ Ghafula nilikuwa katika Roho, hapo mbele yangu kilikuwapo kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu mmoja. Yeye aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua ulioonekana kama zumaridi. Piakukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti ishirini na vinne na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne, waliovaa majoho meupe, wakiwa na taji …..” (Ufunuo 4: 1-4).
Sehemu kubwa ya kitabu cha ufunuo wa Yohana ni maono kuhusu mambo mbalimbali kama vile Mungu na Mwana Kondoo wa Mungu (4:1-5; 14), vita vya mbinguni na duniani (12:1-14; 20) na mengineyo.
Stefano Mtumishi wa Mungu baada ya kutoa hotuba yake mbele ya kuhani mkuu juu ya Taifa la Israeli tangu kuuzwa Yusufu, utumwani kule Misri, kukombolewa na ukaidi wa wana wa Israeli mbele ya Mungu na jinsi walivyozidi kuwatesa watumishi wa Mungu Biblia inasema kuwa walighadhabika na kumsagia meno Stefano. Katika hali ngumu akiwa amejaa na Roho Mtakatifu akatiwa nguvu kwa kuona maono ya Ki-Mungu;
“Waliposikia haya wakaghadhibika, wakamsagia Stefano meno. Lakini yeye (Stefano) akiwa amejazwa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, naye Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.’’ Lakini wao wakapiga kelele Kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja. Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. …”(Matendo 7:54-58).
Paulo, Timotheo na Sila walikataliwa na Roho Mtakatifu kwenda kuhubiri kule Bethania na hivyo wakapita mpaka kule Troa ambako wakati wa Usiku Mungu alisema na Paulo kwa maono waende kuhubiri kule Makedonia ndipo wakajiandaa kwenda huko kwa uhakika;
“Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa. Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia ukatusaidie.” Baada ya Paulo kuona maono haya, mara tulijiandaa kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kwa sababu tuliona kwa hakika kwamba Mungu ametuita kuhubiri habari njema huko” (Matendo 16:8-10).
Zakaria naye alipata kuona maono mbalimbali kama inavyojidhihirisha katika maandiko Matakatifu; Zakaria aliona maono nane, mawili yake ni haya;
”Wakati wa usiku nilipata maono, mbele yangu alikuwepo mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia na weupe. Nikauliza, ‘‘Hivi ni vitu gani bwana wangu?’’ Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, ‘‘Nitakuonyesha ….’’ (Matendo 1:8-9).
Kisha nikatazama juu, na pale mbele yangu nikaona pembe nne! Nikamwuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Ni nini hivi?’’ Akanijibu, “Hizi ni zile pembe zilizowatawanya Yuda, Israeli na Yerusalemu.’’ Kisha BWANA akanionyesha ….” (Matendo 1:18-20).
Ili upate kuona maono ya ki-Mugu ni lazima uwe katika hali ya utakatifu katika maisha yako na kwamba uwe katika Roho na mnyenyekevu kwa ajili ya utukufu wa Bwana. Kumbuka usipokuwa mwaminifu, shetani naye anaweza kuleta mono yake na kusababisha kuharibiwa kwa kanisa na hii ndiyo sababu ya kulazimika kayapima (kuyajaribu) maono.
Hakuna sababu ya kuona halafu kusiwe na maana yake, hivyo upatapo maono mwombe sana Mungu akuongoze kufahamu maana yake, vinginevyo hakuna faida yake.
Njia hii pia imetumika sana katika kujulisha watumishi wa Mungu shida na mahitaji ya watu mbalimbali kama vile magonjwa, njaa, kukosa mavazi n.k. Kwa mfano, katika kusanyiko mtumishi ghafla anajisikia sehemu fulani ya kiungo cha mwili kumuuma, basi hutambua kuna mtu hapo ambaye sehemu hiyo ya mwili inamuuma au wakati mwingine anajisikia njaa ghafla basi atajua kuna mwenye uhitaji wa chakula n.k. Hizi ni hali ambazo hujitokeza kwa muda mfupi na ni hali ambazo kwa kawaida unakuwa huna isipokuwa Roho Mtakatifu anakuwa amezileta kwako kwa ajili ya kulijenga kanisa kwa njia ya kuwaombea wahitaji na au kuwashauri kulingana na yeye mwenyewe atakavyokuongoza.
Neno la Mungu linasema:
“Basi kuna aina mbali mbali za karama, lakini Roho ni yule yule. Pia kuna huduma za aina mbali mbali, lakini Bwana ni yule yule. Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote. Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima ….”(1Wakorintho 12:4-8).
Neno hekima (wisdom) lina maana ya uwezo wa kutoa maamuzi yaliyo sahihi na yasiyoleta matatizo katika jamii au kundi la watu. Uwezo huu kwa kawaida hutokana na ufahamu unaotokana na uzoefu wa namna ya kutenda.
Kuna aina mbili za hekima kulingana na Maandiko Matakatifu, yaani hekima ya mbinguni na hekima ya duniani. Angalia;
Lakini miongoni mwa watu waliokomaa (wakamilifu) twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika kwa wanadamu, ambayo Mungu aliikusudia kabla ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu (1Wakoritho 2:6-7).
Paulo anapozungumzia watu waliookoka anamaanisha watu waliookoka (waliotakaswa) na kwamba hao ndio walio na hekima ya mbinguni. Kunapokuwa na wakamilifu maana yake wapo na wasio wakamilifu (wanaobatilika) na kwamba hao ndio walio na hekima ya duniani (ya kibinadamu tu). Maandiko pia yanasema;
“Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni bali ni ya kidunia, ya tabia ya kibinadamu wala si ya kiroho bali ni ya Shetani. Kwa maana panapokuwa na wivu na ugomvi ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna. Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, ya upole, iliyo tayari kusikiliza maneno ya watu wengine, yenye unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena ya kweli” (Yakobo 3:13-17).
Hapa Yakobo anaonesha tofauti iliyopo baina ya hekima ya mbinguni na ya duniani.
Karama ya Neno la Hekima ni tofauti na hekima hizi mbili. Yeyote aliyeokoka anayo hekima ya mbinguni bila kujali ni ya kujaa au ya kupungukiwa. Ndiyo maana tunapopungukiwa tunahitaji kwenda mbele za Mungu kuomba kwa kuamini atujazie. Angalia;
“Kama mtu ye yote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, Yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku”(Yakobo 1:5-6).
Hapa Yakobo anaonesha ilivyo muhimu sana kwa waliookoka kuwa na hekima itokayokwa Mungu (hekima ya mbinguni).
Kwa sababu ya kuwepo karama mbalimbali, basi karama ya Neno la Maarifa wanayo baadhi ya watu kulingana na jinsi Roho Mtakatifu alivyoamua kugawa. Kumbuka hapa kuwa kuna tofauti kati ya karama ya Neno la Hekima na hekima, kwamba kila aliyeokooka hupewa hekima kutoka mbinguni lakini ni baadhi tu watu hao hupewa Karama ya Neno la Hekima. Mara nyingi hekima ya duniani huhitaji ushahidi ili kufanya maamuzi.
Karama ya Nano la Hekima ni matamshi ya hekima yanayosemwa kupitia utendaji wa Roho Mtakatifu. Huleta ufunuo wa Neno la Mungu au hekima ya Roho Mtakatifu kwa tukio maalum au tatizo na hapo hakuna awezaye kuishinda.
“Stefano, akiwa amejawa na neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa la ‘Watu Huru,’ (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wakirene, Waiskanderia na wengine kutoka Kilikia na Asia, wakasimama na kujadiliana na Stefano. Lakini hawakuweza kushindana na hekima na Roho ambaye kwayo alisema” (Matendo 6:8-10).
Neno la hekima linakuja kwa kulisoma Neno la Mungu kwa bidii na kutafakari njia za Mungu na Neno lake, na kwa kuomba.
“Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonyesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka katika watu Mataifa kwa ajili ya jina lake. Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa: ‘Baada ya mambo haya nitarudi…’ “Kwa hiyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwasumbue watu Mataifa wanaomgeukia Mungu kwa desturi zetu, badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe tu na vitu vilivyotiwa unajisi na uasherati na wasile nyama za wanyama walionyongwa au kunywa damu”” (Matendo 15:14-20).
Hapa Paulo alifanya maamuzi kulingana na Maandiko Matakatifu juu ya mila na desturi zilizokuwa zikiwasumbua Wayahudi dhidi ya waamini wapya. Hili ni Neno la maarifa na ni kwa sababu alikuwa amesoma Neno la Mungu.
Karama ya Neno la Hekima hutenda kazi kwa ufunuo wa Mungu. Hivyo Neno la Hekima huja kwa mtu kwa kufunuliwa na Mungu. Tuangalie baadhi ya Vifungu vya Biblia kuhusiana na utendaji kazi wake;
Mfalme Sulemani aliwaamua wanawake wawili waliokuwa wakigombaniana mtoto baada ya mmoja kufariki; uamuzi wake ulikuwa wa hali ya juu sana.
Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake. Mmojawapo akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami. Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine ye yote katika nyumba isipokuwa sisi wawili. “Wakati wa usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia. Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu. Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia sana katika nuru ya asubuhi, nilionakuwa hakuwa yule mwana niliyekuwa nimemzaa. Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.’’ Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako, aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme. Mfalme akasema, “Huyu anasema, “Mwanangu ndiye aliye hai na aliyekufa ndiye mwanao, maadam yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako na aliye hai ni wangu.’’ Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga. Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, mpe huyu nusu na mwingine nusu.”Mwanamke ambaye mwanaye alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimue!” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!’’ Kisha mfalme akatoa uamuzi wake: “Mpeni mama wa kwanza mtoto aliye hai. Msimue, ndiye mama yake.’’ Wakati Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki” (1Wafalme 3:16-27).
Maamuzi haya ni ya hali ya juu sana, ya ufunuo wa kutoka kwa Mungu kwa sababu maamuzi haya katika hali ya kawaida yangehitaji kupata ashahidi wa kile kinachodaiwa. Hapa Biblia haioneshi kuwa palikuwa na ushahidi isipokuwa tu Mungu alileta Neno la Hekima kuupata ukweli.
Wakati mwingine mafarisayo walimfumania mwanamke katika uzinzi nao wakampeleka kwa Yesu ili kumjaribu Yesu wapate sababu ya kumshitaki, lakini Yesu kwa Neno la Hekima aliwafanya watoweke na kumwacha mwanamke peke yake na Yesu;
Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote. Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini. Katika sheria, Mose alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, mpaka wafe. Sasa Wewe wasemaje?’’ Walimwuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki. Lakini Yesu akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole Chake. Walipoendelea kumwulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu ye yote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.’’ Akainama tena na kuandika ardhini. Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Yesu akabaki peke Yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele Yake. (Yohana 8:3-9).
Kilichowafanya Mafarisayo na Walimu wa sheria kuondoka ni Neno la Hekima walilolisikia yaani “Kama kuna mtu ye yote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe”; walishtakiwa dhamiri zao kuwa wenye dhambi wasiostahili kumpiga mawe yule mwanamke.
Mfano mwingine ni ule wa Mafarisayo walipotaka kumtega Yesu kuhusiana na kulipa kodi kwa Kaisari ili akosane na serikali;
Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake. Wakatuma wanafunzi wao kwake pamoja na Maherode, wakisema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuonyesha tofauti kwa mtu wala upendeleo. Tuambie basi, Wewe unaonaje? Ni halali kulipa kodi kwa Kaisari au la?” Lakini Yesu akijua makusudi yao mabaya akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? Nionyesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi. “Wakamletea dinari. Naye akawauliza,”Sura hii na maandishi haya ni vya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.’’ Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.’’ Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao (Mathayo 22:13-22).
Kwa Neno la Hekima Yesu aliwajibu mafarisayo kwa namna ya ajabu sana kiasi ambacho isingewezekana kwa akili ya kawaida. Lengo lao laakutaka kumtega na kumshitaki likawa limeshindikana na badala yake wakabaki wanashangaa.
Post a Comment